Zanganeh: Iran haihitaji idhini ya kurejea katika soko la mafuta
(last modified Mon, 14 Dec 2020 12:27:16 GMT )
Dec 14, 2020 12:27 UTC
  • Zanganeh: Iran haihitaji idhini ya kurejea katika soko la mafuta

Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Bijan Namdar Zangeneh amesema taifa hili halihitaji idhini yoyote kurejea katika soko la mafuta na kwamba lina uwezo wa kuuza mapipa milioni 2.3 ya mafuta kila siku.

Zanganeh amesema hayo leo pambizoni mwa hafla ya kuzindua awamu ya 11 ya uchimaji mafuta katika eneo la Pars Kusini katika Ghuba ya Uajemi na kuongeza kuwa, "iwapo hakutakuwa na vikwazo, na rasimali za kuhuisha visima ambavyo vilikuwa vimepunguza uzalishali wake zitarejeshwa, basi uuzaji wa mapipa milioni 2.3 ya mafuta nje ya nchi (kama huko nyuma) unawekezana."

Ameleza bayana kuwa, Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) ina wajibu wa kudhibiti bei ya mafuta katika soko la kimataifa, na kwamba Iran ina haki ya kurejea katika soko la mafuta pasina kumuomba yeyote ruhusa.

Zanganeh ameeleza bayana kuwa, katika kipindi cha vikwazo dhidi ya Iran, Jamhuri ya Kiislamu imeidhihirishia dunia kuwa, kamwe haitakata tamaa, na ikatafuta njia mbadala ya kuhakikisha kuwa kunaendelea kuwepo na ustawi katika sekta ya mafuta.

Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, licha ya vikwazo vya Marekani dhidi ya sekta ya mafuta ya Iran, lakini kamwe taifa hili halijasitisha uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu.