Zarif: Iran haitajadili tena makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i66598-zarif_iran_haitajadili_tena_makubaliano_ya_nyuklia_ya_jcpoa
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema kuwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yalijadiliwa na kukamilika na hayawezi kuzungumziwa tena.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Feb 07, 2021 23:42 UTC
  • Muhammad Javad Zarif
    Muhammad Javad Zarif

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema kuwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yalijadiliwa na kukamilika na hayawezi kuzungumziwa tena.

Muhammad Javad Zarif ambaye jana alikuwa akizungumza na televisheni ya CNN ya Marekani amesema kuwa, Donald Trump aliiondoa Marekani katika mapatano na makubaliano hayo ya nyuklia na rais wa sasa wa Marekani, Joe Biden anapaswa kuirejesha nchi hiyo katika mapatano hayo. Zarif amesisitiza kuwa, Iran haijaondoka katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA bali imepunguza utekelezaji wa baadhi ya vipengee vyake. 

Kuhusu matamshi yaliyotolewa na maafisa wa serikali ya Marekani juu ya kuwepo mazungumzo ya kujadili makombora ya balestiki ya Iran, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema kuwa: Mwaka jana Saudi Arabia ilinunua silaha zenye thamani ya dola bilioni 70, Imarati ikanunua silaha zenye thamani ya karibu dola bilioni 23 licha ya kuwa na jamii ya wenyeji karibu milioni moja na nusu tu. 

Zarif: Mwaka jana Saudia ilinunua silaha za dola bilioni 70 

Javad Zarif ameashiria kwamba Iran ambayo ina jeshi lenye zaidi ya askari rasmi milioni moja imetumia karibu dola bilioni 10 hadi 11 katika masuala ya kijeshi na kusema: Marekani haipaswi kuzungumzia masuala ya kiulinzi ya Iran bali Wamarekani wanapaswa kuzungumzia silaha zote wanazozituma katika eneo la Magharibi mwa Asia ambazo zinatumiwa kuua wanawake na watoto wadogo nchini Yemen.