Iran kuishtaki Marekani Mahakama ya Kimataifa ya ICJ kwa uporaji mali
Rais Hassan Rouhani amesema Iran hivi karibuni itawasilisha lalamiko dhidi ya Marekani katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu ICJ, huko The Hague, kufuatia uamuzi wa mahakama moja ya Markeani kuchukua kwa nguvu dola bilioni mbili za Iran zilizoko nchini humo.
"Serikali kamwe haitaruhusu fedha za taifa la Iran ziporwe kirahisi na Marekani," amesema Rais Rouhani akihutubu leo mbele ya halaiki kubwa ya wananchi katika mji wa Kerman kusini magharibi mwa Iran.
Rouhani ameahidi kuipeleka kesi ya uporaji wa fedha hizo katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu hivi karibuni na kuongeza kuwa hatua zote zitachukuliwa ili kurejesha haki za taifa la Iran kupitia njia za kisheria, kisiasa na kibenki.
Ikumbukwe kuwa tarehe 20 Aprili, Mahakama Kuu ya Marekani ilipitisha uamuzi kuwa, katika kuchunguza madai ya waathirika wa eti makosa ya jinai za ugaidi mahakama za nchi hiyo zinaweza kutumia mali na fedha za Iran zilizozuiliwa nchini humo ili kuwalipa fidia watu hao. Mahakama hiyo ilisema dola bilioni mbili za Iran zilizoko katika benki za Marekani zipewe familia za wanajeshi wa Marekani waliouawa mwaka 1983 katika hujuma ya bomu huko Beirut Lebanon ambayo Iran inatuhumiwa kuhusika nayo. Iran imekana vikali kuhusika na hujuma hiyo na kusema fedha ambazo mahakama ya Marekani imezichukua ni mali ya Benki Kuu ya Iran.