Sisitizo la Rouhani kuhusu kutekelezwa kikamilifu mapatano ya nyuklia na pande zote
Hassan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana Jumapili alikutana na mabalozi na wawakilishi wa Iran katika nchi za kigeni katika kongamano la "Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na Uchumi wa Muqawama; Fursa na Uwezo"
Katika kikao hicho Rais Rouhani amesema mapatano ya nyuklia yanayojulikana kwa kifupi kama JCPOA yanamaanisha kuwa pande zote husika zitekeleze ahadi za mapatano.
Aidha ameashiria matokeo mazuri ya mazungumzo ya nyuklia na kusema, sambamba na kusimama kidete, Iran inapaswa kuimarisha ushurikiano na mataifa mengine na wakati huo huo kuushinikiza upande wa pili katika mapatano utekeleze ahadi zake kikamilifu.
Hakuna shaka kuwa mapatano ya JCPOA ni mafanikio ya sera za kigeni ya serikali katika kuamiliana vizuri na dunia. Kwa msingi huo ni jambo linalotarajiwa kuwa Iran itazamie mapatano hayo ya nyuklia yalete harakati mpya za kiuchumi. Hata hivyo jambo hilo limekabiliwa na vizingiti kadhaa.
Weledi wa mambo ya kisiasa wanaamini kuwa, hatua ya mahakama ya Marekani ya kutoa hukumu dhidi ya Iran katika kesi ambayo haina uhusiano wa moja kwa moja na kadhia ya nyuklia ni mojawapo ya vizingiti katika utekelezwaji kikamilifu wa mapatano hayo. Ikumbukwe kuwa uhusiano wa kibenki ni kati ya nukta muhimu za mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa dunani.
Baadhi ya makundi nchini Marekani yameanzisha wimbi jipya la chuki dhidi ya Iran ili kuzuia kutekelezwa kikamilifu mapatano ya nyuklia. Katika miezi ya hivi karibuni mahakama za majimbo nchini Marekani zimetoa hukumu dhidi ya Iran kuhusuiana na hujuma za kigaidi za Septemba 11 na pia hujuma zinginezo za kigaidi.
Katika hukumu ya hivi karibuni ya mwezi uliopita wa Aprili, mahakama moja ya Marekani ilitoa madai bandia kuwa eti Iran ilihusika na utegaji bomu katika kituo cha jeshi la Marekani mjini Beirut mwaka 1983 na kusema kuwa, Iran ilipe fidia familia za askari waliouawa katika tukio hilo. Iran aidha imetupiwa tuhuma ya kichekesho kuwa eti ilihusika na hujuma za kigaidi za Septemba 11, 2001.
Pamoja na kuwa hatua hizo za mahakama za Marekani zinakiuka sheria za kimataifa, lakini wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imeunga mkono ukiukwaji huo.
Hivi sasa benki nyingi za Ulaya zina wasiwasi kuwa iwapo zitakuwa na maingiliano ya kibiashara na Iran basi zitatozwa faini nzito nzito za Marekani.
Uhasama huo unaendelea wakati ambao John Kerry Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani hivi karibuni alishiriki katika kikao na wakuu wa benki muhimu za Ulaya kwa lengo la kuondoa vizingiti katika maingiliano ya kibenki na Iran.
Pamoja na kuwa katika kikao hicho Kerry alizihakikishia benki za Ulaya kuwa hazitaadhibiwa na Marekani zikifanya biashara na Iran, lakini siku chache zilizopita, benki kubwa ya Uingereza ya HSBC ilitangaza kuwa haina hamu ya kufanya biashara na Iran.
Benki hiyo imesema imechukua hatua hiyo kwa kuhofia kutozwa faini na Marekani. Ni wazi kuwa Marekani inaendeleza vikwazo visivyo vya nyuklia dhidi ya Iran kwa njia mbali mbali kama vile kuzitishia kwa njia isiyo ya moja kwa moja benki za Ulaya na hivyo kuzifanya zisiwe na hamu ya kufanya biashara na Iran.
Matamshi ya Rais Hassan Rouhani wa Iran kuhusu ulazima wa pande zote mbili kutekeleza mapatano ya nyuklia ni jambo linaloashiria nukta hii kuwa, kuna udharura wa kusimama kidete mbele ya uchochezi wa Marekani wenye lengo la kudunisha mafanikio yaliyofikiwa katika mapatano ya nyuklia.