Iran inamiliki teknolojia za kisasa za kijeshi kukabiliana na maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i76924-iran_inamiliki_teknolojia_za_kisasa_za_kijeshi_kukabiliana_na_maadui
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema Iran sasa inamiliki teknolojia za kisasa kabisa za kijeshi na katu haitaruhusu adui atekeleza hujuma yoyote dhidi ya nchi.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Nov 15, 2021 01:23 UTC
  • Iran inamiliki teknolojia za kisasa za kijeshi kukabiliana na maadui

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema Iran sasa inamiliki teknolojia za kisasa kabisa za kijeshi na katu haitaruhusu adui atekeleza hujuma yoyote dhidi ya nchi.

Meja Jenerali Hossein Salami ameyasema hayo Jumapili wakati akikagua suhula za Kikosi cha Majini cha IRGC katika Bahari ya Kaspi kaskazini mwa Iran.

Amesisitiza kuwa, IRGC haitamruhusu adui yeyote athubutu kuishambulia Iran na kuongeza kuwa, kusimama kidete taifa la Iran kumesambaratisha njama za maadui.

Salami ameongeza kuwa, kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, miundo yote ya nguvu na uwezo ya Iran ilikuwa inasimamiwa na madola ajinabi na hivyo nchi ilikuwa tegemezi. Amesema hata hivyo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran imeweza kupata nguvu na teknolojia ya hali ya juu na nukta hii imepelekea maadui waingiwe na woga.

Meja Jenerali Salami amesema hivi sasa Iran imeweza kuimarisha uwezo wake wa kijeshi majini na hivyo imeweza kupania wigo wa satwa yake. Amesema hivi sasa Iran inamiliki teknolojia ya kuunda meli za kisasa za kivita ambazo ni utambulisho halisi wa uwezo wa kijeshi baharini.

Meja Jenerali Hossein Salami

Ikumbukwe kuwa, Mnamo Oktoba 24, meli ya mafuta inayojulikana kwa jina la MV Sothys, ilinaswa na makomando wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika Bahari ya Oman wakati Jeshi la Majini la Marekani lilipokuwa likiisindikiza baada ya kujazwa mafuta yaliyoibwa kutoka meli ya mafuta ya Iran. Jeshi la Majini la Marekani lilikuwa linalenga kuelekeza na kudhibiti mafuta hayo ya Iran yaliyoibwa lakini katika oparesheni maalumu makomando wa Iran wakafanikiwa kuzuia uharamia huo wa Marekani.