Iran yasubiri jibu la Saudia ili kuanza tena mazungumzo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i76934-iran_yasubiri_jibu_la_saudia_ili_kuanza_tena_mazungumzo
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hivi sasa Iran inasubiri Saudia ionyesha nia na irada ya kuanzisha tena mazungumzo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 15, 2021 04:44 UTC
  • Iran  yasubiri jibu la Saudia ili kuanza tena mazungumzo

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hivi sasa Iran inasubiri Saudia ionyesha nia na irada ya kuanzisha tena mazungumzo.

Akizungumza na waandishi habari mjini Tehran, Saeed Khatibzadeh Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyasema hayo alipojibu swali la mwandishi wa Iran Press kuhusu matamshi ya hivi karibnui ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Faisal bin Farhan Al Saud aliyedai kuwa mazungumzo ya Iran na Saudia yamekuwa mazuri.

Khatibzadeh amesema hakuna chochote kipya kilichofanyika katika mazungumzo ya Iran na Saudia. 

Mwezi Oktoba Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema, mazungumzo kati ya Iran na Saudi Arabia ni "muhimu sana".

Stéphane Dujarric ameeleza kwamba, mashauriano yanayofanyika kati ya Saudia na Iran ni muhimu sana; na kwa lugha ya uwazi kabisa ni yenye umuhimu mkubwa sana kwa amani ya eneo.

Faisal bin Farhan

Hivi karibuni Iraq ilitangaza kwamba, inashiriki kama msuluhishi katika mazungumzo ya kuondoa mivutano kati ya Saudia na Iran.

Duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Tehran na Riyadh ilifanyika takribani miezi sita iliyopita huko Baghdad; na baada ya hapo, mji mkuu huo wa Iraq umeendelea kushuhudia duru kadhaa za mazungumzo baina ya maafisa wa nchi hizo mbili.

Mazungumzo hayo yanafanyika katika hali ambayo, Saudi Arabia inatumia kila njia ili kujinasua na kujitoa kwenye kinamasi cha vita vya miaka kadhaa ilivyoanzisha dhidi ya Yemen, vita ambavyo licha ya kupelekea makumi ya maelfu ya raia wa Yemen kuuawa na kujeruhiwa na mamilioni kuwa wakimbizi, havijaweza kufanikisha kufikiwa hata lengo moja la Riyadh na washirika wake.