Iran: Mafanikio ya mazungumzo ya nyuklia yanategemea iwapo vikwazo vitaendelea
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema mafanikio ya mazungumzo ya Iran na kundi la 4+1 yatakayoanza Novemba 29 yatategemea iwapo kutakuwa na irada imara ya upande wa pili ya kuondoa vikwazo au la.
Ali Bagheri-Kani ameyasema hayo katika ujumbe wa Twitter na kusema tayari ameshawafahamisha mabalozi wa kigeni walioko Tehran kuhusu msimamo huo wa Iran.
Katika ujumbe wake Bagheri-Kani amesema Jumatano alikutana na mabalozi wa nchi za Ghuba ya Ujaemi na Ulaya Mashariki na Ukanda wa Mediterranean walioko Tehran na kuwafahamisha kuwa mafanikio ya mazungumzo yatategemea irada ya upande wa pili na utayarifu wa kuondolewa vikwazo.
Wajumbe wa Iran na nchi za 4+1 ambazo ni China Russia, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya wanatazamiwa kukutana Vienna, Austria Novemba 29 kwa ajili ya duru ya saba ya mazungumzo. Ikumbukwe kuwa mazungumzo hayo yalisitishwa June wakati wa uchaguzi wa Iran na sasa baada ya serikali mpya ya Iran kutathamini hali ya mambo, mazungumzo hayo sasa yanatarajiwa kuanza upya.

Russia na China zimesisitiza kwamba mazungumzo ya pande zilizosalia katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA ya mwaka 2015 yatafanikiwa tu iwapo yatapelekea kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran.
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alitangaza kujiondoa katika mapatano ya JCPOA mnamo Mei mwaka 2018 na kisha baada ya hapo akatangaza kurejesha vikwazo vilivyo kinyume cha sheria dhidi ya Iran.