Ubalozi wa Palestina Tehran walaani uhasama wa Uingereza dhidi ya Hamas
Ubalozi wa Palestina mjini Tehran umetoa taarifa na kulaani vikali hatua ya Uingereza ya kuiweka Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika orodha ya makundi ya 'kigaidi'.
Taarifa hiyo imesema badala ya uhasama huo serikali ya Uingereza inapaswa kutambua rasmi uhuru wa Palestina.
Aidha Ubalozi wa Palestina mjini Tehran umesema nchi ambazo zinatambua taifa la Palestina ni zaidi ya nchi ambazo zimeutambua utawala wa Kizayuni wa Israel. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Uingereza ndio chanzo cha matatizo ya taifa la Palestina kwa muda wa miaka 73 sasa.
Ikumbukwe kuwa, katika kuendeleza siasa zake dhidi ya taifa la Palestina na kuunga mkono utawala haramu wa Israel, Uingereza imetuhumu na kuitangaza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Paletina Hamas kuwa ni kundi la kigaidi.
Ijumaa iliyopita Priti Patel, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza wa Chama cha Wahafidhina alitoa taarifa na kupiga marufuku shughuli za harakati hiyo nchini humo. Huku akikariri tuhuma zisizothibitishwa dhidi ya Hamas, Patel alisema: 'Hamas ina uwezo mkubwa wa kigaidi zikiwemo silaha nyingi za kisasa na vilevile suhula za mafunzo ya ugaidi na ndio maana leo nimeamua kupiga marufuku shughuli zake hapa nchini.'
Uamuzi huo wa Uingereza unaendelea kulaaniwa kieneo na kimataifa.