Iran: Nchi tatu za Ulaya kuweni na insafu kama mnataka kushirikiana nasi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameziambia nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwamba uungwana ni kuwa na insafu katika mambo yao.
Saeed Khatibzadeh amesema hayo usiku wa kuamkia leo Alkhamisi katika mtandao wa kijamii wa Twitter ikiwa ni kujibu tamko jipya la nchi hizo tatu za Ulaya ambazo zimejaribu kuonesha kuwa Iran ndiye mkosa katika hali yaliyo nayo hivi sasa mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kurefuka mazungumzo ya Vienna yanayojadili makubaliano hayo ya kimataifa.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu tamko la nchi hizo tatu za Ulaya za Uingereza, Ujerumani na Ufaransa na kusema, tamko lolote kuhusu mapatano ya JCPOA ambalo litafumbia macho makosa ya Marekani ambayo ndiyo iliyojitoa kwenye makubaliano hayo, tamko hilo halibainishi chochote isipokuwa upeo wa ujinga wa wanaotoa taarifa kama hiyo.

Khatibazadeh vile vile amesema, kama nchi hizo tatu za Ulaya zinataka kuwa mshirika muadilifu na mwenye insafu, basi hazina budi kuonesha kivitendo insafu yao.
Vile vile ameandika: Kwa Iran mapatano ya JCPOA yalipoteza thamani kuanzia ile siku ambayo upande wa pili uliposhindwa kuheshimu ahadi zake kwa Tehran ndani ya makubaliano hayo. Inabidi manufaa ya Iran kwenye JCPOA yaheshimiwe na yadhaminiwe, ameandika.
Awamu mpya ya mazungumzo ya JCPOA baina ya Iran na kundi la 4+1 ilianza rasmi siku ya Jumatatu ya tareh 29 Novemba mjini Vienna Austria na yanaendelea hadi hivi sasa licha ya nchi za Ulaya kujaribu kupotosha ukweli wa mambo.