Iran yamuunga mkono mwalimu Muislamu Canada, yataka marufuku ya Hijabu iondolewe
Afisa mwandamizi wa masuala ya haki za binadmau nchini Iran ameitaka serikali ya Canada ifute sheria ya kibaguzi ambayo imepelekea mwalimu Muislamu afutwe kazi kwa sababu tu alivaa vazi la Hijabu ndani ya darasa katika mkoa wa Quebec mashariki mwa nchi hiyo.
Fatemeh Anvari, mwalimu wa darasa la tatu katika mji wa Chelsea nchini Canada alifutwa kazi kama mwalimu mapema mwezi huu kwa sababu alikuwa ameavaa mtandio kinyume cha sheria ya kibaguzi iliyopitishwa mwaka 2019.
Kufutwa kazi mwalimu huyo kumelaaniwa vikali kote Canada na hasa Quebec huku wakosoaji wakisema sheria hiyo ni ya kibaguzi.
Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter, Kazem Gharibabadi, Mkuu wa Ofisi ya Haki za Binadamu Iran amesema: "Tunatoa wito kwa serikali ya Canada iingilie kati katika kesi hii na ifute sheria hiyo kama njia ya kuwaunga mkono Waquebec wanaopinga sheria hiyo ya kibaguzi."
Jimbo la Quebec ambalo wakazi wake wanazungumza Kifaransa, lilipitisha sheria hiyo dhidi ya Hijabu mwaka 2019 kwa kisingizio cha kuunga mkono msingi wa usekulari katika sekta ya huduma za umma.
Sheria hiyo inawapiga marufuku wafanyakazi wa sekta ya umma Canada wakiwemo maafisa wa polisi, majaji na walimu kuvaa nembo za kidini wakiwa kazini. Sheria hiyo imekuwa ikiwalenga zaidi wanawake Waislamu wanaovaa Hijabu.
Jumuiya ya Asasi za Uhuru wa Kiraia Canada pamoja na Baraza la Kitaifa la Waislamu Canada zitashirikiana na makundi mengine katika kufikisha kesi mahakamani mwaka ujao kupinga sheria hiyo ya Quebec.
Uislamu ni dini inayoenea kwa kasi zaidi Canada ambapo Waislamu wameongezeka kwa asilimia 82 katika kipindi cha muoongo mmoja uliopita. Hivi sasa Waislamu ni karibu asilimia 3.5 ya watu wote milioni 38 nchini Canada. Kutokana na hali hiyo kumekuwepo jitihada za makusudi za kueneza chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.