Mafanikio mazuri yamepatikana katika mazungumzo ya Vienna
Kiongozi wa ujumbe wa Iran katika mazungumzo ya kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran huko Vienna amesema hatua nzuri zimepigwa na kuongeza kuwa, mazungumzo hayo yatasitishwa kwa siku kadhaa.
Katika ujumbe wa Twitter Ijumaa asubuhi, Ali Bagheri Kani amesema: "Kufuatia mashauriano na wajumbe wengine, jana nimekutana na Enrique Mora kujadili hali ilivvyo na njia ya kufuata."
Enrique Mora ni Naibu Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya na ni mratibu wa mazungumzo ya Vienna.
Duru ya saba ya kikao hicho cha JCPOA ilianza tarehe 29 mwezi uliopita wa Novemba katika mji mkuu wa Austria, Vienna. Mazungumzo hayo ni baina ya Iran na nchi za kundi la 4+1 kuhusu kuondolewea vikwazo, hasa vya Marekani dhidi ya Iran. Nchi za 4+1 ni China Russia, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya.
Ujumbe wa Iran katika mazungumzo hayo unaongozwa na Ali Baqeri, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni anayeshughulikia masuala ya kisiasa.

Ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unashiriki katika mazungumzo huko Vienna kwa mujibu wa haki yake ya kisheria katika fremu ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kile inachotaka ni kuondolewa vikwazo vyote kwa njia ambayo itaweza kuthibitishwa kivitendo.
Wakuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamesisitiza mara kadhaa kwamba, lengo kuu la Tehran la kushiriki mazungumzo ya Vienna kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni kuhakikisha kuwa taifa hili linaondolewa vikwazo vyote haramu.