Iran: Marekani ndio iliyokwamisha mchakato wa mazungumzo ya Vienna Austria
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiiislamu ya Iran ameashiria mazungumzo ya nyuklia ya Vienna Austria na kusema kuwa, hati ya makubaliano hayo ipo tayari kwa ajili ya kusainiwa, lakini Marekani ndiyo iliyokwamisha mchakato huo.
Saeed Khatibzadeh, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiiislamu ya Iran amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya Televisheni ya al-Manar na kubainisha kwamba, kumefikiwa makubaliano kuhusiana na maudhui za mazungumzo ya Vienna na kinachosubiriwa ni pande husika kutia saini, lakini Marekani ndiyo inayokwamisha mambo katika baadhi ya vipengee.
Amesema kuwa, Marekani haiwezi kuchukua maamuzi ya kisiasa katika masuala hayo na kuongeza kwamba, inasikitisha kuona kuwa, serikali ya Rais Joe Biden badala ya kuthibitisha nia njema iliyonayo, imekuwa ikitanguliza mbele misimamo ya serikali iliyotangulia ya Donald Trump.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, hata leo kama Marekani itachukua maamuzi muhimu katika masuala machache yaliyobakia, basi Iran iko tayari kurejea hata kesho katika meza ya mazungumzo huuko Vienna.

Duru ya 8 ya mazungumzo ya kuiondolea Iran vikwazo, ambayo ilianza Disemba 27, 2021, iliingia katika hatua muhimu mnamo Machi 11, 2022, kwa pendekezo lililotolewa na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya (EU), Joseph Borrell, na timu zinazoshiriki mazungumzo zimerudi kwenye miji yao mikuu kwa mashauriano ya kisiasa.
Wakati huo huo, Iran na Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuwa mapumziko ya muda mrefu si kwa maslahi ya mazungumzo hayoi ya Vienna.