Amir-Abdollahian: Mazungumzo ya Vienna hayajasitishwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa mazungumzo ya nyuklia ya Vienna hayajakwama.
Duru ya 8 ya mazungumzo ya nyuklia yenye lengo la kuiondolea Iran vikwazo, ambayo ilianza Disemba 27, 2021, iliingia katika hatua muhimu mnamo Machi 11, 2022, kwa pendekezo lililotolewa na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya (EU), Joseph Borrell, na timu zinazoshiriki mazungumzo zilirudi kwenye miji yao mikuu kwa mashauriano ya kisiasa.
Tokea wakati huo hadi sasa, pande husika katika mazungumzo hayo, yaani kundi la nchi za 4+1 ambazo ni Iran kwa upande mmoja na China, Russia, Uingereza, Ufaransa pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya kwa upande wa pili zimekuwa zikizungumza kuhusu kupunguza hitilafu. Kilichobakia ni kuwaondoa watu na taasisi katika orodha ya vikwazo na Marekani, kama nchi iliyokiuka na kujiuondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, haijachukua maamuzi ya kisiasa kuhusu kadhia hii.
Ni kwa msingi huo ndio Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mahojiano na Televisheni ya Al Masirah ya Yemen akatangaza kuwa mazungumzo hayo ambayo yamekuwa yakifanyika Vienna, Austria yangali yanaendelea.
Akibainisha nuka hiyo amesema: "Mazungumzo ya Vienna hayajasitishwa, bali mchakato wa kuondolewa vikwazo vya upande mmoja na vya kulazimishwa dhidi yetu umekuwa ukiendelea kwa kubadilishana jumbe za maandishi na Marekani kupitia mwakilishi wa Umoja wa Ulaya."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema lengo la mazungumzo hayo ni kufikiwa mapatano yenye nguvu na ya kudumu na kuongeza kuwa: "Sisi tumeitaka Marekani iondoe vikwazo katika sekta zote na itoe dhamana za kiuchumi. Hizi ndizo nukta zinazojadiliwa katika mazungumzo."
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo na Al Masirah, Amir-Abdolahian amesema ana yakini kuwa Marekani inafahamu vyema mistari miekundi ya Iran na kusisitiza kuwa mazungumzo yataendelea.
Katika mahojiano hayo, Amir-Abdollahian aidha amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima itaendelea kuunga mkono Palestina. Aidha amesema Iran inaunga mkono uundwaji wa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Quds Tukufu au Jerusalem na kwamba kuswali katika Msikiti wa Al Aqsa mjini humo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu itakayotimia kwa damu ya mashahidi wa muqawama na taifa la Palestina.