Iran kupeleka mahujaji karibu 40,000 katika msimu wa Hija mwaka huu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i83310-iran_kupeleka_mahujaji_karibu_40_000_katika_msimu_wa_hija_mwaka_huu
Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kislamu katika masuala ya Hija na Ziara amesema kuwa, mwaka huu karibu raia 40,000 wa Iran watakwenda kutekeleza ibada tukufu ya Hija.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 06, 2022 03:09 UTC
  • Iran kupeleka mahujaji karibu 40,000 katika msimu wa Hija mwaka huu

Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kislamu katika masuala ya Hija na Ziara amesema kuwa, mwaka huu karibu raia 40,000 wa Iran watakwenda kutekeleza ibada tukufu ya Hija.

Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Abdul Fattah Navab alisema hayo jana baada ya kuonana na Maayatullah Naser Makarim Shirazi, Hossein Nour Hamedani na Jafar Sobahani katika mji mtukufu wa Qum na kuongeza kuwa, mwaka huu mahujaji 39,600 wa Iran watakwenda kutekeleza ibada ya Hija katika maeneo matakatifu ya Makka na Madina.

Mwakilishi huyo wa Kiongozi Mkuu wa kidini nchini Iran amegusia pia masharti yaliyowekwa na Saudi Arabia ya kuitaka Iran ipelekea asilimia 45 tu ya mahujaji mwaka huu tena walio na umri wa chini ya miaka 65 na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tayari imeiandikia barua serikali ya Saudi Arabia na kuipa mapendekezo yake kuhusu kuongezwa idadi ya mahujaji wa Iran na kupandishwa pia umri wa mahujaji yaani kuruhusiwa kuhiji hata walio na zaidi ya miaka 65 akisema kuwa, ana matumaini mamlaka za Saudia zitazingatia mapendekezo hayo ya Iran.

Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah

 

Kwa upande wake, Sayyid Sadeq Hosseini, Mkuu wa Taasisi ya Hija na Ziara ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, ndege ya kwanza ya mahujaji itaelekea nchini Saudi Arabia kutokea Iran tarehe 13 Juni mwaka huu wa 2022 na ndege ya mwisho kuelekea nchini humo kwa ajili ya ibada ya Hija itasafiri tarehe 28 mwezi huo wa Juni tukijaaliwa.

Mahujaji hao wote ni wale waliotimiza masharti yakiwemo ya kupiga chanjo kamili za kujikinga na ugonjwa hatari wa UVIKO-19 yaani corona.