Makomandoo wa Iran wazima hujuma ya maharamia Ghuba ya Aden
Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetangaza kuwa makomandoo wa jeshi hilo wamezima hujuma ya maharamia dhidi ya meli ya kibiashara ya Iran katika Ghuba ya Aden.
Kwa mujibu wa taarifa, meli hiyo ya mizigo ya Iran ilishambuliwa Ijumaa asubuhi na maharamia wasiojulikana na baada ya kuomba msaada wa dharura, manowari ya kivita ya Iran iliyokuwa karibu ilifika haraka eneo la tukio na kupambana na kuwatimua maharamia.
Meli hiyo ya mizigo ya kibiashara ya Iran sasa inaelekea ilikokuwa ikienda baada ya kunusuriwa na makomando hao ambao wako katika Msafara wa 80 wa Manoari za Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mwezi Oktoba mwaka jana pia meli ya kivita ya Iran ilizima hujuma ya maharamia dhidi ya meli ya mafuta ya Iran katika Ghuba ya Aden baada ya ufyatulianaji risasi na maharamia.
Tokea mwaka 2008, Jeshi la Iran limekuwa likilinda doria katika Ghuba ya Aden ili kulinda meli za mizigo na meli za mafuta za Iran na za nchi zingine. Hatua hiyo ya Iran kutuma meli zake katika eneo hilo ni kwa mujibu wa jitihada za kimataifa za kukabiliana na maharamia.
Tokea wakati huo Iran imefanikiwa kuzima hujuma kadhaa za maharamia dhidi ya meli zake na zile za kigeni.
Hivi sasa Msafara wa 80 wa Manowari za Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uko katika Bahari ya Hindi na Ghuba ya Aden kwa lengo la kusindikiza meli za mafuta na kibiashara. Kati ya meli za kivita za Iran zilizoko katika msafara huo ni Alborz na Bushehr. Aghalabu ya maharamia katika eneo la Ghuba ya Aden wanatoka Somalia, nchi ambayo imekuwa ikikumbwa na vita vya ndani tokea mwaka 1992.