Rais wa Iran yuko safarini Oman kwa lengo la kuimarisha uhusiano
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i83928-rais_wa_iran_yuko_safarini_oman_kwa_lengo_la_kuimarisha_uhusiano
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo yuko safarini nchini Oman kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili jirani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 23, 2022 02:59 UTC
  • Rais wa Iran yuko safarini Oman kwa lengo la kuimarisha uhusiano

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo yuko safarini nchini Oman kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili jirani.

Akizungumza kabla ya kuondoka uwanja wa ndege wa Tehran kuelekea Muscat mapema leo asubuhi, Rais wa Iran amesema safari yake nchini Oman inafanyika kwa msingi wa kuimarisha uhusiano na nchi jirani. Amesema mazungumzo yake na wakuu wa Oman yatahusu kustawisha uhusiano wa pande mbili na pia wa kieneo.

Rais Raisi ameongeza kuwa ameelekea Oman kufuatia mwaliko rasmi wa Sultan Haitham bin Tariq Al Said na kuongeza kuwa kuna uhusiano wa kirafiki na kidugu baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman.

Aidha amesema nchi mbili zina irada ya kuimarisha zaidi uhusiano katika sekta za biashara, uchukuzi na mawasiliano, nishati, utalii na hasa utalii wa kiafya.

Rais Raisi amesema katika safari yake leo nchini Oman, nchi mbili zitatiliana saini mapatano kadhaa ya ushirikiano na kuongeza kuwa, nchi hizi mbili kwa sasa zinashirikiana katika nyanja mbali mbali. Aidha amesema mazungumzo baina ya nchi za eneo yataweza kuleta usalama. Rais wa Iran ameendelea kusema kuwa uwepo majeshi ajinabi katika eneo hausadii hata kidogo katika kuleta usalama bali pia hata unaweza kuwa tishio kwa usalama.

Rais Ebrahim Raisi akiaga kabla ya kuelekea Oman

Wakati huo huo, Rais Ebrahim Raisi ametuma salamu za pongezi na rambi rambi kwa familia ya shahidi Kanali Hassan Sayyad Khodaei. Amemuomba Mwenyezi Mungu amuinue shahidi huyo katika daraja ya juu na kusema, uchunguzi wa tukio hilo utathibitisha kuwa hakuna shaka uistikbari wa kimataifa ulihusika na jinai hiyo.

Jana Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu  IRGC, lilitangaza kuwa mlinzi wa Haram mwenye kuheshimika Kanali Hassan Sayyad Khodaei aliuawa shahidi katika hujuma ya kigaidi ya wapinga Mapinduzi ya Kiislamu na maajenti wa madola ya kiistikbari duniani.

Rais Raisi amesema wale ambao walipata pigo mikononi mwa Walinzi wa Haram wanataka kuonyesha kukata tamaa kwao kwa njia ya jinai kama hiyo.