Iran: Ushirikiano wa kieneo ndiyo siri ya mabadiliko chanya katika ukanda mzima
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Bahari Nyeusi (BSEC) kuwa, kutekelezwa vipengee vya ukanda wa kibiashara wa Ghuba ya Uajemi na Bahari Nyeusi ndiyo siri ya mabadiliko chanya kwenye eneo hili.
Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo leo katika mazungumzo yake na Lazăr Comănescu na huku akitoa pongezi kwa maadhimisho ya miaka 30 ya kuasisiwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Bahari Nyeusi amesema, kuna nafasi kubwa sana ya ushirikiano baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na jumuiya hiyo ukiwemo uwezo wa Iran katika sekta za kupitishia bidhaa na nishati na ametaka fursa hiyo itumiwe vizuri.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kesho Jumatatu itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa baina ya Tehran na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Bahari Nyeusi (BSEC) ambao kaulimbiu yake itakuwa ni malengo ya muda mrefu ya ushirikiano. Mkutano huo utahudhuriwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Bahari Nyeusi, mabalozi wa nchi wanachama, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya ECO pamoja na wakurugenzi wa ngazi za juu wa sekta binafsi na za serikali za Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran vile vile amesema, mkutano wa huo wa kesho Jumatatu ni fursa nzuri ya kujua uwezo na maeneo mazuri zaidi ya ushirikiano baina ya Iran na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Bahari Nyeusi.
Naye katibu mkuu wa jumuiya hiyo amesema katika mazunguzo hayo kwamba mkutano wa kesho utaandaa mazingira mazuri ya kuimarishwa na kutanuliwa wigo wa ushirikiano wa pande hizo mbili.