Kiongozi Muadhamu: Kutegemea uwezo wa ndani ndiyo silaha ya kusambaratisha vikwazo
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, vikwazo ndiyo silaha inayotumiwa na madola ya kibeberu dhidi ya nchi nyingine na kwamba kutengemea uwezo wa ndani ya nchi ndiyo silaha ya kusambaratisha vikwazo hivyo.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisema hayo jana wakati alipoonana na Rais Emomali Rahmon wa Tajikistan na ujumbe alioandamana nao na huku akigusia mambo mengi ya kihistoria, kidini, kiutamaduni na kilugha yanayoyaunganisha mataifa mawili ya Iran na Tajikistan amesema, nchi hizi mbili ni sawa na ndugu wa familia moja.
Kiongozi Muadhamu pia amesema, eneo la kijiografia la Iran lenye sifa za kila namna na ardhi pana na maeneo mengi yenye rutuba, maendeleo ya kisayansi, kiteknolojia, kiviwanda na mashirika na elimu msingi ya Iran pamoja na maji mengi na migodi ya madini ya kila namna huko Tajikistan, ni katika mambo yanayoandaa uwanja mzuri wa kuimarishwa ushirikiano baina ya pande hizi mbili.
Amesema, licha ya kuwa chini ya vikwazo, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kupata maendeleo mazuri katika nyuga tofauti na lau vikwazo visingekuwepo, Iran isingeliweza kupata maendeleo yote hayo kwani vikwazo vimelilazimisha taifa la Iran liamke na kutegemea nguvu na uwezo wake wa ndani.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameashiria safari ya hivi karibuni ya Mkuu wa Majeshi ya Iran huko Tajikistan na kufunguliwa nchini humo kiwanda cha kutengeneza ndege zisizo na rubani na kuongeza kuwa, ushirikiano wa namna hiyo ni muhimu sana kwani leo hii droni ni silaha muhimu ya kulinda usalama wa nchi.
Kwa upande wake, Rais Emomali Rahmon wa Tajikistan ameelezea kufurahishwa kwake na kuonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na ziara yake hapa Iran na kusema kuwa, mazungumzo mazuri yamefanyika baina ya pande mbili kama vile kuimairsha ushirikiano wa kibiashara, kiuchumi na kiviwanda pamoja na masuala ya kieneo kama usalama nchini Afghanistan.