Khatibzadeh: Marekani haijatoa majibu yaliyotarajiwa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Tehran imeshawasilisha rai na mapendekezo yake katika mabadilishano ya jumbe baina yake na Marekani na akaeleza kwamba, Washington haijatoa majibu yaliyotarajiwa.
Saeed Khatibzadeh, ambaye alikuwa akizungumza leo katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari, amegusia matamshi yaliyotolewa na Robert Malley, mjumbe wa serikali ya Marekani katika masuala ya Iran kwamba fursa ya kufikia mapatano ni finyu mno, na akabainisha kuwa, katika mazungumzo ya Vienna mtazamo wa Iran umebainishwa wazi kabisa, kwa hiyo Jamhuri ya Kiislamu haitatoa jibu lolote kwa kauli ambazo lengo lake ni kuvutia uungaji mkono wa ndani.
Khatibzadeh amefafanua kuwa, sababu ya kusita mazungumzo ya Vienna ni kutojibiwa mapendekezo yaliyowasilishwa na Iran na Ulaya, kwa hiyo kinachopasa kufanywa ni kusubiri ili kuona ni wakati gani Marekani itaamua kutangaza uamuzi wake.
Kuhusu ripoti iliyotolewa jana Jumatatu na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran amesema, ripoti hiyo haikuzingatia insafu na kuna mambo ndani ya ripoti hiyo yameelezwa kwa pupa.
Sambamba na kutanabahisha kuhusu hofu iliyopo ya mashinikizo ya wazayuni na baadhi ya pande kuutoa mkondo wa ripoti za IAEA kwenye anga ya kiufundi na kuuelekeza kwenye matashi ya kisiasa, Khatibzadeh amesema, anatumai kuwa mwenendo huo usio sahihi utarekebishwa.../