Aug 25, 2022 03:22 UTC
  • Kan'ani: Iran imepokea jibu la Marekani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza kuwa Iran imepokea jibu la serikali ya Marekani kuhusu mitazamo ya Iran kuhusu kutatua masuala yaliyosalia katika mazungumzo ya kuondoa vikwazo.

Nasser Kan'ani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana Jumatano alitangaza kupokewa jibu la serikali ya Marekani kuhusu maoni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutatua masuala yaliyosalia katika mazungumzo ya kuondoa vikwazo hivyo. Amesema jibu hilo limepokewa kupitia mratibu wa mazungumzo hayo barani Ulaya na kuongeza kuwa: "Baada ya kukamilika uchunguzi kuhusu jibu hilo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itamfahamisha mratibu huyo maoni yake."
Duru mpya ya mazungumzo kuhusu kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, iliyoanza Agosti 4 mjini Vienna, ilimalizika Agosti 8.
Katika duru hii ya mazungumzo, mapendekezo kadhaa yalitolewa na mratibu wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya Vienna.

Enrique Mora mratibu wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya Vienna.

Aghalabu ya nchi zinazoshiriki katika mazungumzo ya Vienna kuhusu kuondolewa vikwazo vya kidhalimu na haramu dhidi ya Iran, zinataka kuhitimishwa kwa haraka mazungumzo hayo. Hata hivyo kufikiwa makubaliano ya mwisho kunasubiri maamuzi ya kisiasa ya Marekani kuhusu mambo machache yaliyosalia ambayo ni muhimu.

Iran iliwasilisha jibu lake kwa pendekezo la rasimu ya Umoja wa Ulaya mnamo Agosti 15, wiki moja baada ya duru ya hivi punde ya mazungumzo kukamilika. Baada ya kuwasilisha majibu yake, Tehran iliitaka Washington izingatie uhalisia wa mambo na ilegeze misimamo ili kufikia makubaliano.

Hata hivyo, ilichukua karibu siku kumi kwa utawala wa Biden kuwasilisha majibu yake kwa maoni ya Iran kuhusu rasimu ya Umoja wa Ulaya.

Marekani, chini ya rais wa zamani Donald Trump, iliachana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mnamo Mei 2018 na kurudisha vikwazo ambavyo makubaliano hayo yalikuwa yameviondoa.

Mazungumzo ya kuokoa makubaliano hayo yalianza katika mji mkuu wa Austria mwezi Aprili mwaka jana, miezi kadhaa baada ya Joe Biden kuchukua nafasi ya Trump. Mazungumzo ya Vienna yamekuwa yakichunguza uwezekano wa Marekani kurejea katika makubaliano hayo na Iran kuondolewa vikwazo vya kidhalimu.

Licha ya maendeleo makubwa katika mazungumzo, hali ya kutokuwa na maamuzi ya Marekani na kuahirisha mambo kulisababisha kukatizwa mara nyingi mazungumzo hayo.

Tags