Raeisi: Vyuo vikuu vimewavunja moyo maadui kwa kuzalisha sayansi na teknolojia
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa vyuo vikuu vya nchi hii vimetoa pigo kwa maadui kwa kuasisi nchi yenye nguvu kupitia uzalishaji wa sayansi na teknolojia na kwamba vyuo vikuu ni jukwaa bora katika uwanja huo.
Akizungumza jana usiku na wakuu wa vyuo vikuu kote nchini Iran, Rais Sayyid Ebrahim Raeisi amevitaja vyuo vikuu kuwa ni vituo vyenye ari na nguvu ambavyo vimewavunja moyo maadui wa Iran kwa kuzalisha uwezo wa nchi kupitia ukuzaji wa sayansi na teknolojia nchini.
Wakuu kadhaa wa vyuo vikuu vya Iran pia waliwasilisha maoni na mitazamo yao katika mkutano huo kabla ya hotuba ya Rais Ebrahim Raeisi.
Rais wa Iran amesisitiza kuwa, ni suala la lazima kwa chuo kikuu kuwa na mazingira ya kisiasa na kwamba chuo kikuu kuwa na utashi wa kisiasa maana yake ni kuwa chuo kikuu kinapasa kuwa na ufahamu mkubwa na bora zaidi kuliko sekta nyingine katika jamii na wakati huo huo kutambua mahitaji na kuainisha vipaumbele vyake katika kuwahudumia wananchi kwa kushirikiana na mifumo mbalimbali ya uendeshaji nchi.
Rais Raeisi wakati huo huo amevitaja vita vya hii leo kuwa ni vita vya hekaya na kusisitiza umuhimu wa kubainishwa simulizi za kweli na sahihi na kusema: adui ambaye anafanya kila awezalo ili kusitisha shughuli za kisayansi, kiviwanda, uzalishaji na huduma mbalimbali nchini na kukata mawasiliano kati ya Iran na nchi nyingine za dunia, huanza kutekeleza njama na ukwamishaji mbalimbali dhidi ya nchi hii pale anapooona amegonga mwamba katika njama zake hizo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya kupanda pakubwa katika uga wa sayansi vyuo vikuu nchini kuwa ni kinyume na matakwa na jitihada za adui za kuitenga Iran na kwamba uhusiano wa Iran na nchi jirani na za kikanda uko katika kupiga hatua.