Kamanda wa IRGC: Tutaharibu usalama wa yeyote atakayedhuru usalama wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89890-kamanda_wa_irgc_tutaharibu_usalama_wa_yeyote_atakayedhuru_usalama_wa_iran
Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ametoa onyo kali kwa maadui, akisema kuwa vikosi vya Iran havina kikomo linapokuja suala la kulinda usalama wa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 31, 2022 03:39 UTC
  • Kamanda wa IRGC: Tutaharibu usalama wa yeyote atakayedhuru usalama wa Iran

Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ametoa onyo kali kwa maadui, akisema kuwa vikosi vya Iran havina kikomo linapokuja suala la kulinda usalama wa nchi.

Brigedia Jenerali Alireza Tangsiri aliyasema hayo jana Jumapili alipokuwa akihutubia kikao cha maafisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Wanamaji la IRGC akimaanisha wazi machafuko ya hivi karibuni kote Iran na shambulio la hivi karibuni la kigaidi lililolenga haram takatifu kusini mwa nchi hiyo.

"Tutaharibu usalama wa yeyote atakayejaribu kudhuru usalama wetu na tutaondoa tishio lolote kwa kufuatialia mzizi wake," Tangsiri amesema.

Akizungumzia shambulio la kigaidi katika mji wa kusini wa Shiraz ambalo lilisababisha waumini 15 kuuawa shahidi, amesema: "Adui alipogundua kuwa shinikizo lake la juu zaidi dhidi ya Iran limeshindwa, alianza kuua raia wetu wasio na hatia."

Hali baada ya hujuma ya kigaidi katika Haram Takatifu ya Shah Cheragh

Waumini 15, akiwemo mwanamke na watoto wawili, waliuawa shahidi na wengine 40 kujeruhiwa baada ya gaidi aliyekuwa na silaha nzito kushambulia Haram Takatifu ya Shah Cheragh huko Shiraz, Mkoa wa Fars, Jumatano kabla ya sala ya jioni. Kundi la kigaidi la Daesh Takfiri limedai kuhusika na shambulio hilo.

Katika ujumbe wake siku ya Alhamisi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei alisema wahusika wa jinai hiyo "ya kutisha" bila shaka watakabiliwa na adhabu.