Rais Raisi: Usalama wa Iran ni mstari mwekundu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89894-rais_raisi_usalama_wa_iran_ni_mstari_mwekundu
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ebrahim Raeisi amesema usalama ni mstari mwekundu kwa serikali yake na kwamba haitaruhusu maadui kuudhoofisha.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 31, 2022 04:03 UTC
  • Rais Raisi: Usalama wa Iran ni mstari mwekundu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ebrahim Raeisi amesema usalama ni mstari mwekundu kwa serikali yake na kwamba haitaruhusu maadui kuudhoofisha.

"Usalama ni mstari mwekundu kwa serikali na taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kamwe hatutaruhusu njama ya adui kudhoofisha rasilimali hii ya kitaifa na yenye thamani," rais wa Iran alisema Jumapili.

Raisi pia amepongeza kujitokeza halaiki kubwa ya wananchi wa Iran kwenye mazishi yaliyofanyika kwa waliouawa shahidi Jumatano katika hujuma ya  kigaidi ya hivi karibuni mjini Shiraz kusini mwa nchi. Akihutubu katika kikao cha baraza la mawaziri, rais wa Iran amesema kilichotokea wakati wa shambulizi katika mji wa Shiraz ni kutimizwa sehemu ya mpango wa adui wa kuzusha ukosefu wa usalama na kuvuruga maisha ya watu kupitia machafuko, ghasia na mauaji.

Ameongeza kuwa, ujumbe mkuu wa mahudhurio ya watu mitaani katika mji wa Shiraz na miji mingine ya Iran haukuwa tu kulaani hujuma ya kigaidi dhidi ya Haram ya Shah Cheragh mjini Shiraz, bali pia ni kubainisha ulazima wa kukabiliana vilivyo na magaidi hao ili kulinda usalama wa nchi.

Wananchi wa Iran katika mazishi ya mashahidi wa hujuma ya kigaidi Shiraz

Waumini 15, akiwemo mwanamke na watoto wawili, waliuawa shahidi na wengine 40 kujeruhiwa baada ya gaidi aliyekuwa na silaha nzito kushambulia Haram ya Shah Cheragh huko Shiraz, Mkoa wa Fars, Jumatano kabla ya Swala ya Magharibi.

Gaidi aliyetekeleza hujuma hiyo alikamatwa na kupelekwa hospitalini baada ya kujeruhiwa katika makabiliano na maafisa wa usalama. Gaidi huyo aliangamia kwa majeraha yake siku ya Ijumaa.

Kundi la kigaidi la Daesh au ISIS limedai kuhusika na shambulio hilo.