Iran yawawekea vikwazo shakhsia 10 na taasisi nne za Marekani
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa imeyaweka majina ya shakhsia kumi na taasisi nne za Marekani kwenye orodha yake ya vikwazo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, wizara ya mambo ya nje ya Iran imeeleza katika taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia leo kuwa, imewawekea vikwazo shakhsia kumi wa Marekani na taasisi nne za nchi hiyo.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewawekea vikwazo shakhsia na taasisi zifuatazo kwa kuendesha harakati zilizo dhidi ya haki za binadamu, kuingilia masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kueneza ghasia na fujo nchini Iran, kuchochea na kuhamasisha vitendo vya kigaidi, kukabiliana na juhudi na harakati za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kupambana na ugaidi na vilevile kuongeza mashinikizo dhidi ya taifa la Iran ambayo ni kielelezo cha ugaidi wa kiuchumi.
Miongoni mwa shakhsia wa Marekani waliomo kwenye orodha hiyo ya vikwazo ni Michael Kurilla, Kamanda wa Kamandi ya Kijeshi ya Kikanda ya Marekani (CENTCOM), Gregory Guillot, Naibu Kamanda wa CENTCOM, Juan Zarate, Mkurugenzi wa Kituo cha Nguvu za Kifedha na Kiuchumi katika Wakfu wa Kutetea Demokrasia na Taasisi ya American Enterprise na Mark Wallace, mkurugenzi mtendaji wa Muungano dhidi ya Iran ya Nyuklia.
Taasisi hiyo ya Muungano dhidi ya Iran ya Nyuklia, Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), Safu ya 9 ya Kikosi cha Anga cha Jeshi la Marekani na Kikosi cha Gadi ya Taifa ya Marekani ndizo taasisi nne zilizomo kwenye orodha ya vikwazo vya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.
Vikwazo walivyowekewa shakhsia hao na taasisi hizo za Marekani ni vya kuzuia utoaji viza na kuingia katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuzuiliwa mali na milki zao katika eneo lililo chini ya mamlaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuzuiwa akaunti zao za benki katika mfumo wa fedha na benki wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.../