Iran yajitosheleza katika uzalishaji wa bidhaa 500 za tiba
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89942-iran_yajitosheleza_katika_uzalishaji_wa_bidhaa_500_za_tiba
Msemaji wa serikali ya Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imeweza kujitosheleza katika uzalishaji wa bidhaa 500 tofauti za tiba.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Nov 01, 2022 07:58 UTC
  • Iran yajitosheleza katika uzalishaji wa bidhaa 500 za tiba

Msemaji wa serikali ya Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imeweza kujitosheleza katika uzalishaji wa bidhaa 500 tofauti za tiba.

Licha ya kuwa chini ya mashinikizo na vikwazo vikubwa kwa zaidi ya miongo minne sasa, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeendelea kuwa imara katika kila upande kwa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kutegemea wananchi wake hasa vijana wenye vipaji vya kila namna. 

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Ali Bahadori Jahromi, Msemaji wa Serikali ya Iran akisema leo Jumanne kwamba, Tehran imefanikiwa kujitosheleza katika uzalishaji wa bidhaa 500 za tiba kama ambavyo imetoa kibali cha kuzalishwa baadhi ya bidhaa hizo nje ya nchi.

Teleskopu ya kisasa 

 

Amesema, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Wairan 2,700 wenye vipaji tofauti wamerejea humu nchini na kwamba hivi sasa zaidi ya Wairan elfu kumi wenye vipawa vya kila namna wanafanya kazi kwa kushirikiana na mashirika ambayo msingi wake ni elimu.

Hii ni katika hali ambayo, mwishoni mwa mwezi ulioisha wa Oktoba, Iran ilitangaza kuwa, wanastronomia wake wameweza kuunda teleskopu ya kiwango cha kimataifa ya mita 3.4 ambayo tayari inafanya kazi na imepata picha zake za kwanza kutoka anga za mbali. Mradi huu wa Kituo cha Kitaifa cha Uangalizi wa Anga za Mbali (observatory) cha  Iran ulianzishwa takriban miaka 20 iliyopita.

Akizungumza na jarida la Kimataifa la Science, Mkurugenzi wa Mradi wa INO Habib Khosroshahi, mwanaastronomia katika Taasisi ya Utafiti wa Sayansi ya Msingi (IPM) mjini Tehran alisema, "Kwa muda mrefu tulikuwa tukisubiri kwa hamu wakati huu."