Eslami: Mafaili ya madai dhidi ya Iran yanapasa kufungwa na vikwazo viondolewe
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesisitiza ulazima wa kufungwa mafaili ya madai yaliyotolewa dhidi ya miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu na kuondolewa vikwazo.
Muhammad Eslami ambaye jana alihojiwa na televisheni na al Mayadeen alieleza kuwa, mafaili ya tuhuma na madai kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran yanapasa kufungwa na vikwazo kuondolewa. Eslami ameongeza kuwa, Iran inaheshimu mapatano ya mwaka 2015 kwa sharti kwamba pande zote pia nazo ziheshimu mapatano hayo.
Duru ya 8 ya mazungumzo ya kuiondolea Iran vikwazo ambayo ilianza Disemba 27 mwaka jana, ilisimama tarehe 11 Machi kufuatia pendekezo la Mkuu wa Sere za Nje wa Umoja wa Ulaya; ambapo timu husika za mazungumzo zilirejea katika miji yao mikuu kwa ajili ya mashauriano zaidi ya kisiasa.
Duru mpya ya mazungumzo ya kuiondolea Iran vikwazo ilianza katika mji wa Vienna, Austria tarehe 4 Agosti mwaka huu baada ya kusita kwa miezi mitano; na kisha mazungumzo hayo yalimalizika tarehe 8 mwezi Agosti mwaka huu baada ya timu za mazungumzo kurejea katika miji yao mikuu.
Nchi nyingi zinazoshiriki katika mazungumzo hayo zinataka kukamilika kwa haraka kwa mazungumzo hayo, lakini kufikia makubaliano ya mwisho kunasubiri maamuzi ya kisiasa ya Marekani kuhusu masuala machache yaliyosalia ambayo ni muhimu na nyeti.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasema kuwa, upo uwezekano wa kufikiwa mapatano huko Vienna iwapo upande wa Marekani utachukua hatua kulingana na uhalisia wa mambo.