Kiongozi Muadhamu: Tarehe 13 Aban inadhihirisha uovu, ukhabithi na kushindwa Marekani
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, tarehe 13 Aban (Novemba 4) ni mfano wa wazi wa uovu, ukhabithi na dhihirisho la kupata pigo na kushindwa Marekani.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo leo mbele ya hadhara ya wanafunzi kwa mnasaba wa kukaribia kumbukumbu ya “Siku ya Kupambana na Ustikbari wa Kimataifa na Siku ya Mwanafunzi hapa Iran na kusisitiza kwamba, 13 Aban ni siku ya kihistoria na wakati huo ho ni siku ya kujipatia na kujifunza tajiriba.
Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, siku hii ni ya kihistoria kwa sababu ilisajili matukio yasiyosahaulika na ambayo hayapaswi kusahaulika na itabakia katika historia kwa sababu inatoa funzo na ibra.
Ayatullah Khamenei amewahutubu wanafunzi hao na kuwataka wajifunze tajiriba hii na mustakabali wao.
Kiongozi Muadhamu amesema kuwa, watu wanaodhani kwamba, Marekani ni nguvu isiyotikisika, tukija na kuangalia na kutupia jicho matukio ya siku hii tunaona kwamba, hapana, dola hilo la kibeberu linaweza kudhurika na kupata pigo.

Ayatullah Khamaenei ameashiria mahesabu kombo ya Marekani katika matukio mbalimbali kama huko Afghanistan na Iraq na kubainisha jinsi siasa za Marekani zilivyojengenga juu ya misingi ya unafiki na kutokuwa na haya wala soni.
Kiongozi Muadhamu ameashiria shambulio la kigaidi la hivi karibuni dhidi ya Haram takatifu ya Ahmad bin Musa (as) huko katika mji wa Shiraz na kueleza kuwa, mauaji dhidi ya wasio na watoto wasio na hatia ni jinai kubwa, hivyo waliohusika na jinai hiyo wanapaswa kutambuliwa na kuadhibiwa pamoja na mtu yeyote ambaye itathibiti alitoa ushirikiano katika jinai hiyo kwa namna moja au nyingine.
Tarehe 13 Aban 1358 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 4 Novemba 1979, wanafunzi wa Chuo Kikuu wa Iran walilivamia pango la kijasusi la Marekani mjini Tehran lililokuwa na ubalozi wa dola hilo la kibeberu baada ya kuongezeka njama za Marekani za kutaka kufanya mapinduzi mengine nchini Iran.