Meja Jenerali Salami: Ndoto ya adui kuitawala Iran kamwe haitatimia
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema: Ndoto ya adui ya kutaka kuitawala Iran ya Kiislamu kamwe haitatimia, bali itaendelea kusalia tu kwenye akili yake ambapo atatumia nguvu zake zote kutaka kuifanikisha bila mafanikio yoyote.
Akizungumza leo Alkhamisi huko katika mji mtakatifu wa Qum (kusini mwa Tehran) Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, adui ana tatizo na falsafa ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, na kusema, vikwazo ambavyo Iran inakabiliwa navyo tangu mwanzo wa uhai wake ni mkakati haribifu zaidi ambao kundi moja la nchi linaweza kutumia dhidi ya taifa jingine, mkakati ambao licha ya adui kushindwa kuufanikisha lakini bado anautumia dhidi ya taifa hili shupavu.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Uwezo wa Iran wa kukabiliana pamoja na kuvunja vikwazo ni fahari ya kitaifa, ambapo leo inakidhi mahitaji yake kwa kutegemea vyanzo vyake vya ndani ya nchi na wala haihitaji wageni ili kuijenga nchi. Baraka na neema zote zinapatikana kwa wingi ndani ya nchi na kwa hivyo Iran haionekani kuwa nchi iliyozingirwa kutokana na vikwazo vya kimataifa na hilo ndilo jambo ambalo linamkasirisha adui.
Meja Jenerali Salami ameendelea kusema: Leo, Iran inaendelea kuimarisha nguvu zake za ndege zisizo na rubani (droni), makombora na uwezo wake wa kijeshi, jambo ambalo halikubaliki kwa adui.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Adui ametumia njia zote lakini hajafanikiwa, kuanzia mzingiro wa kiuchumi hadi vita vya kulazimishwa, kuanzisha pote la ukufurishaji (Daesh), vita vya kisaikolojia, kujaribu kuitenga Iran katika ngazi za kimataifa na kuizuia katika utatuzi wa migogoro ya kikanda; lakini njia zote zimefungwa mbele ya adui na kutokuwa na njia nyingine yoyote ya kuidhuru Iran.