Iran yapinga azimio la muswada wa Canada Baraza Kuu la UN
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i91756-iran_yapinga_azimio_la_muswada_wa_canada_baraza_kuu_la_un
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amekutaja kupitishwa azimio la chuki dhidi ya Iran katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa pendekezo la Canada na kwa uungaji mkono wa nchi za Ulaya na utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni jambo linaloakisi unafiki na sera za kindumakuwili za nchi zilizopendekeza na kuunga mkono muswada wa azimio hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 16, 2022 04:33 UTC
  • Iran yapinga azimio la muswada wa Canada Baraza Kuu la UN

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amekutaja kupitishwa azimio la chuki dhidi ya Iran katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa pendekezo la Canada na kwa uungaji mkono wa nchi za Ulaya na utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni jambo linaloakisi unafiki na sera za kindumakuwili za nchi zilizopendekeza na kuunga mkono muswada wa azimio hilo.

Nasser Kan'ani amesema azimio hilo halina hadhi wana uhalali.

Azimio dhidi ya Iran la muswada uliopendekezwa na Canada, ambalo huwasilishwa kila mwaka kwa kisingizio cha haki za binadamu, liliidhinishwa kwa kura 80 za ndio, kura 29 za kulipinga na 65 zimekataa kupiga kura katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hii ina maana kwamba nchi 94 hazikukubaliana na azimio hilo dhidi ya Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran, Nasser Kan'ani, amesema mapema leo Ijumaa kwamba sera za kinafiki za watayarishaj wa azimio hilo katika kutumia taasisi za kimataifa kama chombo cha kuiwekea mashinikizo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni mfano wa wazi wa dhulma ya kutumia vibaya matukufu ya haki za binadamu ili kuendeleza malengo yao ya kisiasa.

Kanani ameashiria juhudi za nchi za Magharibi za kuendeleza mradi wa propaganda chafu za kueneza chuki dhidi ya Iran na vita vya kisaikolojia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kusema: Watayarishaji wa azimio dhidi ya Iran ambao wao wenyewe ni wakiukaji wakuu wa misingi yote ya awali kabisa ya haki za binadamu duniani, wanapaswa kuacha kuunga mkono ugaidi wa kiuchumi wa serikali ya Marekani dhidi ya taifa la Iran na kutokuwa mwenyeji wa makundi ya kigaidi  badala ya kuonyesha huruma ya kinafiki kwa eti haki za binadamu za watu wa Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya kigeni ya Iran amesisitiza kuwa, uzingatiaji wa haki za binadamu ni moja ya misingi na kidini na kisheria ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu siku zote imekuwa na nia ya dhati ya kuboresha haki za binadamu na kutekeleza majukumu yake ya kimataifa, na iko tayari kufanya mazungumzo na ushirikiano wenye kujenga katika fremu ya kuheshimiana, kutobaguana, uadilifu na insafu ili kuboresha haki za binadamu duniani bila ya kuhusisha kadhia hiyo na masuala ya kisiasa.