Iran yavunja mtandao wa kijasusi wa Mossad uliolenga sekta yake ya ulinzi
Wizara ya Intelijensia ya Iran imetambua na kuwatia mbaroni wanachama wa mtandao wa kijasusi waliokuwa wanapanga kuhujumu sekta ya ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia mashirika na masoko yanayouza bidhaa za kiusalama.
Shirika la habari la Tasnim liliripoti jana Jumapili kwamba maafisa wa usalama wa Iran wamefichua njama ya mtandao huo wa kijasusi wa Mossad ya kukusanya taarifa kutoka kwa mashirika ya Iran yenye msingi wa elimu, ambayo yanashirikiana na sekta ya ulinzi humu nchini.
Ripoti hiyo inasema Shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel Mossad, lilimwajiri dalali wa data Frank Genin, ambaye alijitambulisha kama mkuu wa shirika la kutengeneza vipuri na kuweza kuwasiliana na mashirika na wafanyakazi kadhaa wa Iran.
Dalali huyo wa Mossad kisha aliwaalika wafanyakazi wenzake kwenye semina huko Malaysia, ambako aliwatambulisha kwa jasusi mwingine wa Mossad kwa jina la Hadrien Lavaux.
Ili kuficha utambulisho wake, Lavaux amekuwa akifanya kazi kama mkurugenzi mkuu wa shirika linalojiita Triple A Industries, linalojishughulisha na masuala ya anga na ambalo lilianzishwa nchini Singapore mnamo 2017. Tangu wakati huo, shirika hilo lilianza kuwasiliana na mashirika ya Iran.
Washirika wa Lavaux nchini Iran walihudhuria maonyesho tofauti, wakafuatilia mikutano ya kisayansi na kutambua mahitaji ya sasa ya sekta ya ulinzi ya Iran.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadaye majasusi hao walianza kuwafuatilia wakuu, wauzaji na wafanyakazi muhimu wa mashirika ambayo yanashirikiana na sekta ya ulinzi ya Iran. Wakuu na wafanyakazi hao walialikwa kwenye mikutano kadhaa iliyofanyika katika nchi za Uturuki, Hungary, Oman na Georgia, na safari zao kugharamiwa kikamilifu na majasusi hao wa Mossad.
Hata hivyo, maafisa wa usalama wa Iran walikuwa vikifuatilia kwa karibu safari hizo na hivyo kuweza kuujua zaidi mtandao huo.
Mossad imeongeza shughuli zake za ujasusi nchini Iran katika miezi ya karibuni ambapo imehusika na vita vya siri dhidi ya Iran kwa kuunga mkono mashambulizi ya kigaidi na ghasia katika pembe tofauti za nchi.
Maadui wa Iran na hasa utawala wa kibaguzi wa Israel na Marekani, wamekuwa wakishiriki katika operesheni za kujasusi na kuhujumu sekta ya ulinzi ya Iran.
Nguzo muhimu ya mkakati wa ulinzi wa Iran ni makombora yake ambayo sasa yameimarishwa kiteknolojia na kufikia kiwango cha makombora ya Hypersonic ambayo yanakwenda kwa mwendo wa mara 5 hadi 25 zaidi ya kasi ya sauti.
Iran imetambua umuhimu wa kujitosheleza kijeshi kwa zaidi ya miongo minne ya vikwazo, kikiwepo kipindi cha vita vya kulazimishwa vya miaka minane vya Iraq, wakati nchi zenye nguvu duniani zilikataa kuiuzia Iran hata nyaya za miba, achilia mbali silaha.
Jamhuri ya Kiislamu inasisitiza kuwa kwa kuzingatia stratijia ya kudumu ya Washington ya kutumia vitisho vya kijeshi dhidi ya Tehran, Iran haina budi ila kuimarisha uwezo wake wa kiulinzi.