Kan'ani: Nchi za Magharibi zimepata hasara kwa kuunga mkono ghasia Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan’ani, anasema nchi za Magharibi zilifanya mahesabu vibaya na zimepata hasara kwa kuunga mkono ghasi za hivi majuzi katika maeneo kadhaa ya Iran.
Kan’ani ameuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Tehran siku ya Jumatatu kwamba nchi za Magharibi tayari zimekiri makosa yao kuhusiana na machafuko yanayoendelea nchini Iran.
"Serikali zinazoweka dau kuhusu matukio ya ndani ya Iran huweka dau juu ya farasi aliyeshindwa.
Ameongeza kuwa, ingawa serikali za Magharibi zinadai kwamba hazikuwa zikifuatilia mabadiliko ya utawala nchini Iran, lakini Tehran haitasahau kamwe kuhusika kwao katika ghasia hizo."
Kan’ani pia ameashiria suala la raia wa kigeni wanaozuiliwa kwa kuhusika katika ghasia hizo, akisema Tehran tayari imeshaziarifu nchi zao, na wengine waliruhusiwa hata kuwasiliana na familia zao, kama ishara ya ubinadamu wakati wa siku kuu ya Krismasi.
Siku ya Jumatatu pia, Kan’ani kwa mara nyingine tena amepuuzilia mbali madai yasiyo na msingi kwamba Iran iliipatia Russia ndege zisizo na rubani zinazotumika katika vita vya Ukraine, akisema kuwa maafisa wa Iran na Wizara ya Mambo ya Nje wamekanusha mara kwa mara madai hayo.

Kwingineko katika matamshi yake, msemaji huyo amesema Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikiliweka wazi dirisha la diplomasia kwa ajili ya kuhuisha mapatano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Amesema kuokoa makubaliano ya nyuklia ya 2015 bado kunaweza kufikiwa ikiwa upande wa Magharibi utaonyesha nia ya kweli.
Ameutaja mkutano wa hivi karibuni kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian na Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya katika Masuala ya Kigeni na Sera ya Usalama Josep Borrell kuwa ni tukio muhimu na fursa nzuri kwa pande zote mbili.