Meja Jenerali Salami: Adui alishindwa katika matukio ya hivi karibuni
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i92232-meja_jenerali_salami_adui_alishindwa_katika_matukio_ya_hivi_karibuni
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu akizungumzia machafuko ya hivi karibuni nchini Iran amesema, adui aliingia uwanjani kwa nguvu zake zote katika matukio ya hivi karibuni, lakini akashindwa vibaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 28, 2022 23:21 UTC
  • Meja Jenerali Salami: Adui alishindwa katika matukio ya hivi karibuni

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu akizungumzia machafuko ya hivi karibuni nchini Iran amesema, adui aliingia uwanjani kwa nguvu zake zote katika matukio ya hivi karibuni, lakini akashindwa vibaya.

Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa licha ya maadui kutumia mbinu zao zote na kuingia uwanjani wakiwa na uwezo wao wote pamoja na kutumia uzoefu wote waliokuwanao lakini wameshindwa kufikia malengo yao maovu dhidi ya mfumo wa Kiislamu.

Meja Jenerali Salami ameongeza kuwa, kama Iran isingekuwa na uzoefu  ilioupata huko nyuma, ingeshindwa kusimama mbele ya vitisho vya wakati mmoja na vya mfululizo vya maadui.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kuwa leo moto wa mgawanyiko unawaka kwenye kambi ya maadui na kuongeza kwamba maadui wanahasimiana wazi, wameshindwa na wana hasira kubwa.

Ghasia za karibuni mjini Tehran

Kuibuka machafuko ya hivi karibuni nchini Iran kwa kisingizio cha kifo cha Mahsa Amini kwa mara nyingine tena kuliwapelekea maadui wa kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuitumia kama fursa nzuri ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran na kuzusha machafuko nchini kadiri walivyoweza.

Katika ghasia za hivi karibuni, viongozi wa kisiasa wa Marekani na wa Ulaya, kupitia vyombo vyao vya habari na vilevile vyombo vya habari vya lugha ya Kifarsi vinavyoungwa mkono na kudhaminiwa na nchi za Magharibi, walitumia vibaya tukio la kusikitisha la kifo cha Mahsa Amini kudai kutetea kauli mbiu eti ya kuunga mkono haki za watu wa Iran, ambapo walitumia vibaya hali hiyo kuwaunga mkono wafanyaghasia, magaidi na wahuni walioharibu mali za umma. Wakati huo huo, mamilioni ya wananchi wa Iran walijitokeza mitaani, kwenye medani na katika pembe tofauti za nchi kuunga mkono mfumo wa Kiislamu na nchi yao na kupinga vikali machafuko hayo.