Jan 28, 2023 02:32 UTC
  • Jibu la Iran kwa vikwazo vya Umoja wa Ulaya

Katika kukabiliana na vikwazo vya hivi karibuni vya Umoja wa Ulaya, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechapisha orodha mpya ya shakhsia na taasisi za Ulaya ambazo zimewekewa vikwazo na serikali ya Tehran.

Orodha hiyo iliyochapishwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran siku ya Jumatano, inajumuisha majina ya taasisi na makampuni 3, maafisa 22 wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, pamoja na taasisi moja na maafisa 8 wanaohudumu au waliowahi kuhudumu katika serikali ya Uingereza. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran inaeleza kuwa, watu na taasisi zilizojumuishwa katika orodha hiyo ni kutokana na kuhusika kwao kwa njia moja au nyingine katika kuunga mkono ugaidi na makundi ya kigaidi, kuchochea na kuhimiza vitendo vya kigaidi na ukatili dhidi ya wananchi wa Iran, kuingilia masuala ya ndani ya Iran, kueneza ghasia na machafuko nchini Iran, kuchapisha na kutangaza habari za uwongo dhidi ya Iran, na pia kushiriki katika njama za kuongeza vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Wairani, jambo ambalo linachukuliwa kuwa ni ugaidi wa kiuchumi dhidi ya taifa la Iran.

Hatua hii ya Iran ni jibu la vikwazo vya hivi karibuni vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya na Uingereza dhidi ya baadhi ya wabunge, maafisa wa mahakama, jeshi, utawala na utamaduni wa Iran.

Hossein Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Siku ya Jumatatu Umoja wa Ulaya ulitangaza kuidhinisha kifurushi cha nne cha vikwazo dhidi ya Iran, katika Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje la Umoja huo, kwa kisingizio cha kutoheshimiwa haki za binadamu. Kwa mujibu wa vikwazo hivyo vipya, orodha ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran imeongezeka na kufikia watu 173 na taasisi 31.

Kufuatia matukio ya miezi ya hivi karibuni na kuibuka machafuko katika baadhi ya miji ya Iran, Umoja wa Ulaya na nchi za Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Marekani na Canada zimechukua hatua za uhasama dhidi ya Iran, jambo linalothibitisha wazi siasa za kudumu za nchi hizo kutumia vibaya kila fursa inayojitokeza kwa ajili ya kutoa mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi dhidi ya Iran.

Baada ya kushindwa mipango yao ya kisiasa na kipropaganda ya kueneza ghasia na machafuko nchini Iran, pande za Magharibi zikiwemo za Ulaya sasa zinajaribu kuzidisha mashinikizo dhidi ya serikali ya Iran kwa kuongeza vikwazo vya kiuchumi kwa kisingizio eti cha kutetea haki za binadamu, ili zichochee baadhi ya makundi na vibaraka wao ndani ya nchi kwa madhumuni ya kuendeleza ghasia nchini.

Hii ni pamoja na kuwa, kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hatua za uhasama za Wamagharibi katika kutekeleza vikwazo na kuingilia masuala ya ndani ya Iran, hazitawasaidia chochote na wala hazitaifanya Iran isalimu amri mbele ya matakwa yao yasiyo ya kimantiki na ya mabavu.

Iran imekuwa chini ya vikwazo tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na tangu mwaka 2018, wakati serikali ya Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump ilipojitoa katika mapatano ya JCPOA, Iran imewekewa vikwazo vikali zaidi, lakini pamoja na hayo haijalegeza msimamo wala kubadilisha siasa zake za msingi hata chembe katika miaka hii yote, jambo ambalo limewafanya maadui hao wa Magharibi kutofikia malengo yao dhidi ya mfumo wa Kiislamu wa Iran.

Mazungumzo ya JCPOA

Iran imethibitisha kivitendo kwamba haitokubali kudhalilishwa na kuwa itatoa jibu muwafaka kwa hatua zozote haribifu za vikwazo za Wamagharibi na hiyo ndio maana imeamua bila kusita kuwawekea vikwazo mara kadhaa maafisa, taasisi na makampuni ya Marekani, Ulaya na Canada.

Hossein Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Ufaransa siku ya Jumatano, alikosoa misimamo na hatua zisizo za kiujenzi za Bunge la Ulaya na kusema: "Msirudie tena siasa zilizofeli za vikwazo vya Trump, na leo sisi pia tumetangaza orodha mpya ya vikwazo dhidi ya Umoja wa Ulaya na Uingereza, ambayo inajumuisha maafisa na taasisi 34 za Ulaya, kama hatua ya kulipiza kisasi."

Tags