Iran yasaini hati 20 za ushirikiano na nchi za Afrika Magharibi
Maafisa wa ngazi za juu wa Iran wamesema kupanua uhusiano na nchi za Kiafrika ni moja ya sera kuu za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu.
Viongozi wa Iran wamesema hayo katika Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano wa Sayansi na Uchumi baina ya Iran na nchi za Afrika Magharibi ulioanza jana Jumatatu hapa mjini Tehran. Mawaziri, mabalozi, na wawakilishi wa sekta za biashara, nishati na viwanda wa Iran na nchi za Afrika Magharibi wanahudhuria mkutano huo wa siku tatu.
Mohammad Mokhber, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kusainiwa hati 20 za ushirikiano katika nyuga tofauti zikiwemo za kisiasa, kiuchumi, kibiashara na kiutalii katika siku ya kwanza ya mkutano huo baina ya Jamhuri ya Kiislamu na mataifa hayo ya Afrika kunaonesha azma na irada ya kisiasa ya pande mbili ya kuimarisha uhusiano na maingiliano yao.
Mokhberi amesema kufanyika mikutano na vikao vya mara kwa mara vya kamisheni za pamoja za Iran na Afrika Magharibi kutapiga jeki mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi baina ya pande mbili hizo.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, serikali ya awamu ya 13 ya Rais Ebrahim Raisi itafanya kila iwezalo kukuza na kustawisha zaidi ushirikiano wake na mataifa ya Kiafrika.
Amebainisha kuwa, mabadilishano ya kibiashara baina ya Iran na nchi za Afrika Magharibi yanaunda asilimia 40 ya biashara zote baina ya Iran na bara Afrika, na kwamba kuna haja ya kunyanyua juu zaidi kiwango hicho.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Reza Fatemi, Waziri wa Biashara na Madini wa Iran ambaye pia alizungumza kwenye mkutano huo unaowaleta pamoja mawaziri, mabalozi, na wawakilishi wa sekta za biashara, nishati na viwanda wa Iran na Afrika Magharibi.