Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu yapongeza mapatano baina ya Iran na Saudia
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imepongeza mapatano ya kurejesha tena uhusiano wa kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia na kueleza kuwa, hiyo ni hatua muhimu katika uga wa kuimarisha amani na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi.
Gazeti la al-Sharq limemnukuu Hussein Ibrahim Taha, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) akipongeza hatua hiyo na kuashiria sisitizo la Tehran na Riiyadh la kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala mataifa na kutoingiliwa katika masuala yao ya ndani.
Kadhalika Katibu Mkuuu wa OIC amesema, hatua iliyofikiwa na Iran na Saudia ya kurejesha tena uhusiano wao wa kidiplomasia ni muhimu, inayofaa kupongezwa na bila shaka itasaidia mno kuimarisha amani na uthabiti wa eneo la Asia Magharibi.
Makubaliano hayo yaliafikiwa Ijumaa katika mji mkuu wa China, Beijing, baada ya siku kadhaa za mazungumzo magumu kati ya Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran (SNSC) Ali Shamkhani na mwenzake wa Saudia.
Kurejeshwa kwa uhusiano huo kulitangazwa rasmi katika taarifa ya pamoja ya Iran, Saudi Arabia na China siku ya Ijumaa.
Mapatano hayo yalisainiwa na Shamkhani, Musaid Al Aiban, Waziri wa Nchi na mjumbe wa Baraza la Mawaziri wa Saudi Arabia ambaye pia ni Mshauri wa Usalama wa Taifa, na Wang Yi Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamisheni Kuu ya Mambo ya Nje ya Chama cha Kikomunisti cha China.
Saudi Arabia ilikata uhusiano wa kidiplomasia na Iran mnamo Januari 2016 baada ya waandamanaji wa Iran, waliokasirishwa na hatua ya Saudia kumyonga ngozi mashuhuri wa Kishia Sheikh Nimr kuvamia ubalozi wake mjini Tehran na ubalozi mdogo wa Riyadh mjini Mash'had.