Iran: Mashambulizi ya Israel dhidi ya Aleppo yanakiuka sheria za kimataifa
Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amelaani mashambulizi ya anga ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Aleppo (Halab) huko kaskazini mwa Syria na kusisitiza kuwa, uvamizi huo unakanyaga sheria za kimataifa, Hati ya Umoja wa Mataifa mbali na kuwa tishio kubwa kwa amani na uthabiti wa eneo la Asia Magharibi.
Zahra Ershadi alisema hayo jana Alkhamisi akihutubia kikao cha kujadili 'Hali ya Mashariki ya Kati' katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, baraza hilo linapasa kuushinikiza utawala wa Kizayuni ili uhitimishe chokochoko na hatua zake za uvamizi dhidi ya mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Syria.
Ershadi ameeleza kuwa, inasikitisha kuona jamii ya Kimataifa ingali inaendelea kunyamazia kimya wimbi hilo la jinai, mashambulizi ya kigaidi na unyama wa Wazayuni unaofanyika kwa mpangilio maalumu dhidi ya taifa hilo la Kiarabu.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa, "Utawala wa Israel, kwa kufuata sera yake ya uvamizi na ugaidi, ulitekeleza mashambulizi kadhaa ya anga dhidi ya Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Aleppo mnamo Machi 7, na kulemeza huduma zake kwa muda. Shambulizi jingine la kigaidi limefanyika jana tu (juzi Machi 22)."

Kabla ya Aleppo kukabiliwa na mradi wa uasi ulioanza kutekelezwa na maadui mwaka 2011, ulichukuliwa kuwa mji mkuu wa kiuchumi wa Syria. Mji wa Aleppo ulinawiri sana kiuchumi kabla ya maadui kuanza kutekeleza mradi wa kuiangusha serikali halali ya Rais Bashar al-Asad na hilo lilitokana na mapatano mazuri ya kiuchumi na ujirani mwema yaliyokuwa yakitekelezwa kabla ya njama hizo.
Hivi karibuni pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hossein Amir-Abdollahian alilaani wimbi hilo la mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Syria, wakati huu ambapo taifa hilo linakabiliwa na matatizo chungu nzima kutoka na maafa makubwa ya matetemeko ya ardhi yaliyoua maelfu ya watu, mbali na kusababisha mamilioni ya wengine kukosa makazi.