Hussein Amir-Abdolllahian: Oman ni jirani na rafiki wa kuaminika wa Iran
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Oman ni jirani na rafiki wa kuaminika wa Iran na kwamba, mashirikiano baina ya mataifa haya mawili yataongezeka na kuimarika zaidi.
Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazunguuzo yake kwa njia ya simu na Badr bin Hamad al-Busaidi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Oman na kusisitiza kwamba, daima Muscat imekuwa jirani na rafiki wa kuaminika wa Tehran.
Mazungumzo mawaziri hao wa mashauri ya kigeni wa Iran na Oman mbali na kujadili masuala ya uhusiano wa pande mbili na namna ya kuimarisha ushirikiano baina yao, yaliangazia pia matukio ya kieneo na kimataifa.
Kwa upande wake Badr bin Hamad al-Busaidi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Oman amesema kuwa, mataifa ya eneo hili la Asia Magharibi yanaweza kufupisha njia ndefu ya ustawi na maendeleo ya eneo hili kwa kudumisha ushirikiano baina yao.
Licha ya kuweko hali tete kwenye eneo la Ghuba ya Uajemi katika miongo kadhaa iliyopita na pamoja na kuwepo njama kubwa za Marekani na maadui wenzake za kueneza chuki dhidi ya Iran, lakini daima uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Oman ni wa kuheshimiana na kuchunga manufaa ya pamoja.
Viongozi wa Oman wanaamini kwamba, kuwa na uhusiano mzuri na Iran ni katika kuangalia mambo katika uhalisia wake kwani Iran ni jirani mwenye nguvu ambaye haiwezekani kabisa kudharau kuwa na uhusiano nayo.
Viongozi wa Iran nao muda wote wamekuwa wakitilia mkazo wajibu wa kushirikiana vilivyo nchi jirani na kutotoa mwanya wa kuvamiwa eneo lao na madola ajinabi yasiyoyatakia kheri mataifa ya eneo hilo.