Sheikh Naim Qassim: Makubaliano ya Iran na Saudi Arabia yalikuwa ya kishujaa
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni baina ya Iran na Saudi Arabia ya kuanzisha tena uhusiano wao wa kidiplomasia yalikuwa ya kishujaa.
Sheikh Naim Qassim sambamba na kuashiria kwamba, hivi sasa eneo la Asia Magharibi linaelekea upande wa amani na uthabiti ameyasifu makubaliano ya Iran na Saudia yaliyofikiwa kwa upatanishi wa China.
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ameisifu hatua hiyo ya Iran na Saudia na kubainisha kwamba, makubaliano hayo yamefikiwa kwa kuwa Riyadh na Tehran zinataka kushirikiana baina yao na kuweka muongozo wao kwa ajili ya kuleta uthabiti wa kisiasa wa nchi zao na eneo hili la Asia Magharibi.
Aidha ameongeza kuwa, kile kilichofikiwa baina ya Iran na Saudia kimebadilisha muelekeo wa Asia Magharibi na kwa mara nyingine tena utawala haramu wa Israel umekuwa adui wa kweli wa watu wote.
Wakati wa mazungumzo kati ya Iran na Saudi Arabia yaliyofanyika mjini Beijing, China mnamo Machi 10 nchi hizo mbili zilikubaliana baada ya kupita miaka saba kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia.
Alireza Enayati, Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya Ghuba ya Uajemi katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran alisema hivi karibuni kwamba, kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa, balozi za Iran na Saudi Arabia zitafunguliwa tena ifikapo tarehe 9 Mei 2023, na imepangwa pia kuwa Mashauri ya Kigeni wa nchi hizo mbili watakutana kabla ya kipindi hicho.