Kikao cha pande nne cha Moscow kuhusu Syria pamoja na matokeo yake
(last modified Thu, 11 May 2023 11:24:45 GMT )
May 11, 2023 11:24 UTC
  • Kikao cha pande nne cha Moscow kuhusu Syria pamoja na matokeo yake

Kikao cha kwanza cha pande nne cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia, Syria, Uturuki na Iran kuhusiana na Syria kilifanyika Jumatano ya jana huko Moscow mji mkuu wa Rusia.

Mwishoni mwa mkutano huo kulitolewa taarifa ya mwisho na washiriki. Taarifa ya mwisho ya Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia, Syria, Uturuki na Iran imetilia mkazo juu ya kuheshimiwa ardhi yote ya Syria, kutoingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na kuandaliwa Ramani ya Njia kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la uhusiano baina ya Uturuki na Syria.

Aidha washiriki wa kikao hicho wamekubaliana kwamba, manaibu mawaziri wa mashauri ya kigeni wa nchi hizo nne wapatiwe jukumu la kuandaa Ramani ya Njia kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la uhusiano wa Uturuki na Syria kwa kufanya uratibu na wizara za ulinzi na wakuu wa mashirika ya kiintelijensia ya mataifa hayo.

Hii ni mara ya tatu kwa Moscow kuandaa mkutano kuhusiana na Syria. Kikao cha kwanza katika kiwango cha manaibu mawaziri wa mashauri ya kigeni na wawakilishi maalumu wa Russia, Iran, Uturiki na Syria kilifanyika tarehe 3 na 4 na za mwezi uliopita wa Aprili katika mji mkuu wa Russia Moscow na Sergei Lavrov Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia alihudhuria mkutano huo katika siku ya pili na ya mwisho na ikakubaliwa kwamba, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni pia wa nchi hizo nne wakutane Moscow.

Baada ya hapo, tarehe 25 Aprili pia mawaziri wa ulinzi na maafisa wa ngazi za juu wa usalama wa nchi hizo nne wakakutana mjini Moscow na kubadilishana mawazo kuhusiana na masuala mbalimbali.

Sergei Lavrov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Rusia amesisitiza kuwa, mwenendo wa kurejeshwa katika hali ya kawaida uhusiano wa Damascus na Ankara ambapo washiriki wake ni majuimui ya nchi washiriki wa mazungumzo ya Astana, una taathira kubwa mno sio tu katika mwenendo wa hali ya Syria kwa ujumla, bali hata kwa anga jumla ya eneo la Asia Magharibi.

Kurejeshwa uhusiano wa kawaida na Syria au nchi zingine za Kiarabu na Uturuki ni jambo ambalo limechukua kasi katika miaka ya hivi karibuni. Kurejea Syria katika nchi za Kiarabu na kuwa na nafasi yake ambapo nembo ya hilo ni kurejeshewa kiti chake cha katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kushiriki tena katika vikao vya kawaida vya jumuiya hiyo ni hatua ambayo inaonyesha kuweko harakati ya pamoja ya nchi za Kiarabu kwa ajili ya kurejesha uhusiano wa kawaida na Damascus baada ya kushindwa mpango wa pamoja wa Waarabu na Wamagharibi wakiongozwa na Marekani uliokuwa ukilenga kuiangusha serikali ya Rais Bashar al-Assad.

Miezi michache baada ya kuanza mgogoro wa Syria, tarehe 12 Novemba 2011, baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Qatar na Saudi Arabia zilitoa mwito wa kusimamishwa uwanachama wa Syria katika mikutano ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Kisingizio kilichotolewa na nchi hizo kuondoa kiti cha Syria katika mikutano ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kilikuwa ni tuhuma kwamba serikali ya Damascus inawakandamiza raia wake. Baadhi ya nchi za Kiarabu zilisimamisha na kufunga ofisi zao za uwakilishi wa kisiasa na hata balozi zao ndogo nchini Syria.

Hivi sasa, baada ya kupita karibu miaka 12 tangu ulipoanza mgogoro huo na kushindwa kwa kampeni kubwa ya kuipindua na kuisambaratisha serikali halali ya Syria na rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad kuweza kuendelea kubaki madarakani, Jumuiya ya Waarabu, katika mkutano wake wa ngazi ya mawaziri, ilichukua uamuzi rasmi wa kuondoa usitishaji wa uwanachama wa Damascus na kuridhia kurejea Syria kwenye jumuiya hiyo. Juhudi hizi zilianzishwa tangu miaka miwili nyuma, ambapo kwa muda wote huo suala la kurejea Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu limekuwa likizungumziwa na kukaririwa mara kwa mara.

Baada ya kushindwa vibaya makundi ya kigaidi nchini Syria, madola ya Kiarabu yamediriki ukweli huu kwamba, kuendeleza siasa zao dhidi ya Syria ambazo hazikuzaa matunda katika kipindi cha muongo mmoja cha kuitenga Syria hakuna faida yoyote kwa mataifa hayo. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana zimeamua kubadilisha sera na msimamo wao kuhusiana na Syria. Serikali ya Uturuki nayo imefikia natija hiyo hiyo iliyofikiwa na mataifa ya Kiarabu. Hivi sasa taifa hilo linafanya juhudi za kurejesha uhusiano wake na Syria kupitia kikao cha pande nne.

Inaonekana kuwa, kwa sasa mpango wa Marekani ni kuzuia kufikiwa uamuzi wa kuanzisha tena uhusiano wa kawaida baina ya Uturuki na Syria. Kwani Washington inatambua vyema kwamba, kama Ankara na Damascus zitapatana na utawala wa Syria ukadhibiti maeneo ambayo hadi sasa yanadhibitiwa na makundi ya kigaidi sambamba na kuondolewa wasiwasi wa Ankara juu ya harakati za magaidi katika maeneo ya mpaka wa nchi mbili hizo, uwepo usio wa kisheria wa Marekani nchini Syria utakabiliwa na kibarua kigumu.