Sultani Haitham wa Oman awasili nchini na kulakiwa rasmi na Rais Raisi
Hafla rasmi ya kumkaribisha Sultani Haitham Bin Tariq Al Saeed wa Oman, ambaye ametembelea Iran kwa mara ya kwanza akiwa Mfalme wa Oman, imefanyika katika jumba la kiutamaduni na kihistoria la Saad Abad hapa mjini Tehran.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Iran IRNA, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Seyed Ebrahim Raisi, ameongoza hafla hiyo rasmi ya kumlaki na kumkaribisha Sultani wa Oman ambayo imeambatana na kupigwa nyimbo za taifa za nchi mbili; na baada ya hapo viongozi hao wa Iran na Oman wakakagua gwaride la heshima na kutambulishana jumbe na maafisa wa pande mbili.
Mazungumzo ya faragha kati ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Sultani wa Oman yamepangwa kufanyika baadaye leo.
Mnamo mwezi Mei mwaka jana, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifanya ziara ya kuitembelea Oman akiongoza ujumbe wa ngazi za juu kwa mwaliko wa Sultani Haitham wa nchi hiyo kwa lengo la kustawisha uhusiano katika nyanja za biashara, uchukuzi, nishati, utalii, na hasa utalii wa afya.
Sultani Haitham Bin Tariq Al Saeed wa Oman aliwasili mjini Tehran leo jioni akiongoza ujumbe wa ngazi za juu. Kwa mujibu wa ofisi kuu ya Usultani ya Oman, ziara ya kiongozi huyo hapa nchini Iran ni ya siku mbili na inalenga kuimarisha uhusiano wa kirafiki uliopo kati ya mataifa hayo mawili.
Ziara ya leo ya Sultani wa Oman mjini Tehran, ambayo ni ya kuitikia ziara ya mwaka jana ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Muscat, inaweza kuwa na taathira kubwa katika kuendeleza mapatano yaliyofikiwa na kuzidisha uhusiano wa kina uliopo kati ya nchi mbili; na bila shaka kuendelea kwa mwenendo wa kirafiki uliopo kati ya Tehran na Muscat kutakuwa na manufaa si kwa watu nchi hizo mbili pekee, lakini kama ilivyokuwa huko nyuma, kwa watu na nchi za eneo hili pia.../