Balozi wa Iran: Israel inataka kuvuruga uhusiano wa Tehran, Riyadh
Balozi mpya wa Iran nchini Saudi Arabia amesema Israel imekerwa na kuhamakishwa na hatua ya kuhuishwa uhusiano wa kidiplomasia wa Tehran na Riyadh, na kwamba utawala huo wa Kizayuni umeazimia kuuvuruga uhusiano huo.
Alireza Enayati amesema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Alam na kuongeza kuwa, mataifa rafiki ya Iran yamekaribisha kwa mikono miwili kitendo cha kufufuliwa uhusiano wa Iran na Saudia.
Jumanne wiki hii, ubalozi wa Iran nchini Saudi Arabia ulifunguliwa tena ikiwa ni miezi mitatu baada ya makubaliano ya kurejeshwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Katika mapatano hayo yaliyofikiwa kwa upatanishi wa China, nchi hizi mbili zilikubali kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia baada ya kukatwa kwa miaka saba.

Enayati amesema kufunguliwa tena ubalozi wa Iran nchini Saudi Arabia ni hatua mpya kuelekea kurejesha uhusiano wa kawaida wa kisiasa na kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili muhimu za Asia Magharibi katika Ghuba ya Uajemi na kuwa msingi wa kustawisha uhusiano kati ya nchi hizo katika nyanja zote.
Balozi mpya wa Iran nchini Saudia ameeleza kuwa, jambo la msingi hivi sasa baada ya kuhuishwa uhusiano huo, ni nchi mbili hizi kuwa na ushirikiano madhubuti, na kutoa kipaumbele kwa suala la usalama wa eneo, kwa misingi ya kustawisha uhusiano wa kiuchumi, kibiashara, kijamii na kitamaduni.