Jul 03, 2023 02:50 UTC
  • Admeri Tangsiri: Mafuta yaliyoko Ghuba ya Uajemi ni ya Iran, majirani zake

Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesema mafuta yaliyoko katika eneo la Ghuba ya Uajemi ni milki ya Iran na majirani zake katika eneo hili la kistratajia.

Admeri Alireza Tangsiri alisema hayo jana katika mahojiano na shirika la habari la Mehr na kusisitiza kuwa, vikosi vya SEPAH vitaendelea kulinda maslahi ya taifa la Iran katika eneo la Ghuba ya Uajemi, ambalo lina umuhimu mkubwa kama mojawapo ya njia muhimu zaidi za baharini.

Amebainisha kuwa, visiwa vitatu vya Abu Musa, Tunb Kubwa na Tunb Ndogo daima vitabaki kuwa vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kamanda Tangsiri amesisitiza kuwa, visiwa hivyo ni milki ya Iran, na ithibati ya hilo ni nyaraka za kale zikiwemo za Umoja wa Mataifa.

Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, Tunb Kubwa ndicho kisiwa cha kwanza cha Jamhuri ya Kiislamu kilichoko katika Lango Bahari la Hormuz.

Ghuba ya Uajemi

Amekumbusha kuwa, Ghuba ya Uajemi ni moja ya maeneo muhimu sana na yenye thamani kubwa duniani na kuwepo utajiri wa mafuta na gesi kwenye pwani ya eneo hilo.

Admeri Alireza Tangsiri amesisitiza kuwa, mafuta yaliyoko katika eneo la Ghuba ya Uajemi ni milki ya Iran na majirani zake katika eneo hili la Asia Magharibi. Ghuba ya Uajemi imekuwa na nafasi muhimu ya kisiasa na kiuchumi na leo hii, inajulikana kama njia kuu ya maji ya kimataifa duniani.

Tags