Aug 15, 2023 07:36 UTC
  • Nasrullah: Tutairejesha Israel 'enzi za jiwe' ikiingia vitani na Lebanon

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameionya vikali Israel na kusisitiza kuwa, utawala huo wa Kizayuni utarejeshwa nyuma mamilioni ya miaka hadi enzi za jiwe, iwapo utaingia katika vita vipya na Lebanon.

Sayyid Hassan Nasrullah alitoa onyo hilo jana Jumatatu katika hotuba yake aliyoitoa kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 17 tangu utawala haramu wa Israel ushindwe kwa madhila katika vita vya siku 33 na Lebanon mwaka 2006.

Amesema, "Nukta muhimu ni kitu ambacho Lebanon na kambi ya muqawama zitafanya iwapo vita vitaibuka. Viongozi na makamanda wa maadui wanalifahamu vyema hili, lakini wanafuatilia tu upotoshaji kupitia vyombo vya habari, kitu ambacho hakina thamani kwetu."

Sayyid Nasrullah ameeleza bayana kuwa, "Tunawaambia makamanda wa adui kuwa, mkiingia katika vita vipya na Lebanon, mtarejeshwa pia enzi za jiwe."

Amesema miaka 17 baada ya vita na Lebanon, Waisraeli hawajaweza kuijenga upya taswira iliyoharibiwa ya jeshi lao. Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa, jeshi la utawala wa Kizayuni hivi sasa lipo katika udhaifu mkubwa zaidi, na ndio maana wanalenga maeneo yasiyo na ulinzi.

Sayyid Hassan Nasrullah ameeleza kuwa, mrengo wa muqawama hivi sasa upo katika hali bora zaidi, huku Wazayuni wakijificha nyuma ya kuta. 

Tags