Dec 08, 2023 03:19 UTC
  • Mzunguko wa mauaji ya kimbari ya Israel kutoka kaskazini hadi kusini mwa Gaza

Mashambulizi ya mabomu ya fosforasi katika kambi ya Jabalia na mapigano makali kati ya vikosi vya muqawama na wavamizi wa Kizayuni kusini mwa Ukanda wa Gaza ni miongoni mwa habari za hivi punde kuhusiana na Palestina.

Nyumba za Wapalestina katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza ikiwemo kambi ya Al-Nusairat, Khan Yunis na Deir al-Balah zimeshambuliwa vikali karibuni na watendajinai wa utawala wa Kizayuni.

Duru za Palestina zimeripoti kuendelea mashambulio ya utawala wa Kizayuni katika hospitali ya Kamal Adwan, kambi ya Jabalia na mji wa Khan Yunis.

Vyanzo hivyo vimetangaza kuwa makombora 70 yamerushwa na utawala wa Kizayuni kuelekea Hospitali ya Kamal Adwan.

Vyanzo vya Wapalestina pia vimeripoti kushambuliwa kwa mabomu kambi ya Jabalia, ambayo ina zaidi ya familia 100.

Raia wengine zaidi ya 70 wameuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni katika makazi ya watu katika Ukanda wa Gaza.

Mauaji ya kimbari ya Wazayuni dhidi ya watoto na wanawake wa Palestina

Kwa mujibu wa takwimu za hivi punde zilizochapishwa, tangu kuanza operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba, watu 16,248 wa Gaza wameuawa shahidi kutokana na mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni.

Vyanzo vya hospitali huko Gaza pia vimesema kwamba mashirika ya kimataifa yameondoka kaskazini mwa Gaza kwenda kusini mwa ukanda huo kutokana na vitisho vya jeshi la utawala wa Kizayuni.

Moja ya malengo makuu ya utawala wa Kizayuni katika kubadilisha mpango wake wa vita dhidi ya Gaza na kuanzisha mashambulizi ya kiwendawazimu kusini mwa ukanda huo ni kudhibiti mji wa Khan Yunis ambao jina lake linahusishwa na Hamas na Qassam.

Kwa imani ya waliowengi,, nguvu za brigedi za Izzudin  Qassam , tawi la kijeshi la Hamas,  zimekita mizizi huko Khan Yunis, mahali walipozaliwa Mohammad Zaif na Yahya Sanwar.

Kwa kubadilisha uwanja wa vita kutoka kaskazini hadi kusini, utawala wa Kizayuni unafuatilia malengo kadhaa kwa wakati mmoja. Kwanza, kujiondoa katika mkwamo wa vita katika eneo la kaskazini na kuelekeza vyombo vya habari kwenye mafanikio ya vita kusini mwa Ukanda wa Gaza. Lengo la pili ni kufikia Khan Yunis ambacho ni miongoni mwa vituo muhimu vya harakati ya Hamas na tawi lake la kijeshi, na lengo la tatu na la mwisho ni kwamba Wazayuni wanajaribu kutoa mashinikizo ya kijamii dhidi ya Hamas kwa kuongeza uharibifu wa makazi ya raia na maafa ya kibinadamu ya watu wa Gaza.

Pamoja na hayo na kama ilivyoonekana wakati wa kubadilishana mateka, mashambulio ya kikatili, mauaji na uharibifu mkubwa unaofanywa na wazayuni dhidi ya watu wa Gaza sio tu  haujapunguza umaarufu wa Hamas na muqawama miongoni mwa Wapalestina, bali umeuimarisha zaidi na wakati huo huo kuongeza mshikamano wa kitaifa wa Palestina.

Katika uwanja wa vita, ripoti zinazotolewa zinaonyesha kuwa, vikosi vya Palestina vinaendesha mapambano makali na kuwa ngome imara dhidi ya kusonga mbele jeshi la wavamizi kusini mwa Gaza, jambo ambalo limepunguza kasi ya wanajeshi wa Kizayuni kuelekea Khan Yunis.

Saraya al-Quds pekee, tawi la kijeshi la Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, limeweza kulenga na kuwaangamiza maafisa na wanajeshi wengine 9 wa Israel mbali na kuharibu magari na zana zao za kijeshi katika saa 24 zilizopita. Kwa maelezo hayo, idadi ya wanajeshi wa Israel waliouawa tangu kuanza operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa imefikia maafisa na wanajeshi 408.

Jinai na uharibifu wa makusudi wa Wazayuni dhidi ya Wapalestina

Wakiashiria kushindwa jeshi la Israel katika medani ya vita, wachambuzi wa Kizayuni wanaelezea kujiri vita vikali katika eneo la Shujaiyeh huko Gaza.

Kwa upande mwingine, nje ya Palestina, pande mpya za vita zinafunguliwa kila siku dhidi ya utawala wa Kizayuni. Kwa mujibu wa duru za kuaminika katika uwanja huo, makundi ya muqawama katika vitongoji vya magharibi mwa mkoa wa Daraa nchini Syria, karibu na mipaka ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, yameshambulia kwa makombora kambi za kijeshi za utawala wa Kizayuni katika Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu, mashambulio ambayo yalikuwa hayajawahi kushuhudiwa tena katika eneo hilo katika miaka ya hivi karibuni. Hili linathibitisha kuwa jinamizi la muungano na mshikamano wa makundi ya muqawama dhidi ya utawala ghasibu wa Israel linaendelea kuwa kubwa siku baada ya nyingine.