Dec 11, 2023 08:02 UTC
  • Kumbukumbu ya mwaka wa sita wa ushindi dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh nchini Iraq

Desemba 10, 2023, imesadifiana na kumbukumbu ya miaka sita ya ushindi wa Iraq dhidi ya magaidi wa kundi la ISIS au Daesh.

Katika historia yake ya zama hizi, Iraq imepitia siku zilizojaa machungu, ikiwa ni pamoja na zama za utawala wa kidekteta wa Baath. Hata hivyo, moja ya matukio machungu zaidi nchini Iraqi ni kuvamiwa nchi hiyo na magaidi wa Daesh mnamo 2014. Magaidi hao wakufurishaji ambao walichukua theluthi moja ya ardhi ya Iraq, walitenda jinai  za kutisha katika nchi hiyo, tokea mauaji ya halaiki hadi kuchoma moto, kukata vichwa na kuwazika hai raia wa Iraq.

Mara tu Iraq ilipokaliwa kwa mabavu na magaidi hao wa Daesh Ayatullah Sistani, kiongozi mkuu wa Mashia wa Iraq, alitoa fatwa na kutangaza kuunda harakati ya wapiganaji wa kujitolea wa wananchi wa Iraq maarufu kama Al Hashd al Shaabi ili kupambana na magaidi hao.

Wapiganaji wa Hashd al Shaabi

Kuundwa kwa Hashd al-Shaabi kulitoa msingi wa kuundwa makundi mengi ya muqawama au mapambano ya Kiisalmu nchini Iraq. Makundi hayo yalikuwa na nafasi muhimu katika vita dhidi ya Daesh na yaliweza kuwatimua magaidi hao kutoka maeneo yote ya nchi hiyo waliyokuwa wameyateka na kuyakalia kwa mabavu. Ingawa jeshi la Iraq na vikosi vya usalama pia vilikuwa na nafasi muhimu katika kutimuliwa magaidi wa Daesh, lakini mwanzoni mwa uvamizi wa Daesh, jeshi la Iraqi lilikuwa karibu kusambaratika na halikuwa na uwezo wa kupambana na magaidi hao wavamizi.

Baada ya mapigano ya miaka mitatu na nusu, hatimaye Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq, Haider al-Abadi, alitangaza ukombozi kamili wa nchi hiyo kutoka kwa makucha ya Daesh mnamo Desemba 10, 2017, na sasa  imepita miaka 6 tangu kupatikana ushindi huo mkubwa.

Karam Saadi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa na kimkakati ya Iraq, ameandika hivi kuhusu suala hilo: "Pengine tukio muhimu zaidi nchini Iraq mwaka 2017 ni kuangamizwa Daesh katika nchi hii.  Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi alitangaza ushindi dhidi ya Daesh baada ya mapigano makali yaliyodumu kwa muda wa miezi 43. Kwa uungaji mkono wa jumuiya ya kimataifa, vikosi vya usalama na kijeshi vya Iraq vilidhibiti maeneo yote yaliyokuwa yanakaliwa na Daesh kwa miaka kadhaa".

Katika taarifa yake kuhusu mwaka wa sita wa ushindi wa nchi hiyo dhidi ya magaidi wa Daesh, Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammad Shia al-Sudani amesisitiza kuwa: "Tunajivunia utendaji wa kishujaa wa vikosi vya jeshi la nchi hii kufuatia Fatwa ya Jihad Kifa'i  iliyotolewa na Ayatullah Seyyed Ali Sistani, marjaa mkuu wa  Mashia wa Iraq, Fatwa ambayo ilipelekea tupate ushindi."

Katika taarifa yake, Rais wa Iraq Abdul Latif Jameel Rashid amewapongeza Wairaqi wote kwa mnasaba wa siku hii na kushukuru kujitolea kwa vikosi vya usalama na jukumu muhimu la viongozi katika kulinda nchi na kuhifadhi heshima yake.

Jambo muhimu kuhusu kushindwa Daesh nchini Iraq ni kwamba, kwa mujibu wa Wairaqi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ilikuwa na nafasi kubwa katika ushindi huo. Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, hayati kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), alikuwa mmoja wa watu waliokuwepo katika uwanja wa mapambano dhidi ya magaidi wa Daesh nchini Iraq pamoja na wenzake wengine.

Shahidi Qassem Soleimani

Mustafa Al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq zama hizo, alikuwa miongoni mwa shakhsia waliothamini nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika vita dhidi ya Daesh. Kuhusiana na hilo, Al-Kadhimi alisema: "Nataka kuwashukuru wale wote waliosimama upande wa taifa la Iraq katika vita dhidi ya magaidi wa Daesh, ambao ni vikosi viovu na Khawarij, na nataka kuishukuru Jamhuri ya Kiislamu iliyosimama na sisi tangu mwanzo katika mapambano dhidi ya Daesh".

Leo, Iraq ina uthabiti na usalama, na vikundi vya kigaidi havina tena uwezo wa kuleta ukosefu wa usalama katika nchi hiyo. Wakati huo huo, makundi ya muqawama au mapambano ya Kiislamu ya Iraq yanafuatilia mapambano dhidi ya Marekani kwa sababu yanasisitiza kuondolewa kabisa jeshi la nchi hiyo katika ardhi yao ili Iraq iweze kuwa huru kikamilifu.

 

Tags