Dec 25, 2023 10:42 UTC
  • Balozi wa Iran: Ulaya ichukue hatua za maana kukomesha mauaji ya kimbari Gaza

Balozi wa Iran nchini Iraq amesema nchi za Ulaya zinapasa kuchukua hatua za maana kwa ajili ya kukomesha jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Mohammad Kazem Al-e Sadeq, Balozi wa Iran mjini Baghdad amesema hayo katika mazungumzo yake na Thomas Seiler, Balozi mpya wa Umoja wa Ulaya nchini Iraq na kuongeza kuwa, nchi za Ulaya zina jukumu la kusimamisha mashambulizi ya kinyama yanayoendelea kufanywa na Israel huko Gaza.

Amekosoa sera za kindumakuwili za madola ya Ulaya yanayodai kuwa yanapigania na kuunga mkono haki za binadamu na kusisitiza kuwa, kuna haja ya kulinda maisha ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina na kuwapa misaada ya kibinadamu.

Balozi wa Iran nchini Iraq ameashiria uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Umoja wa Ulaya na kueleza bayana kuwa, nchi za Ulaya zinapaswa kubadilisha mtazamo wao kwa Tehran na eneo la Asia Magharibi, ili uendane na matukio halisi ya hivi sasa ulimwenguni.

Israel yaendelea kuishambulia Gaza kwa siku ya 80

Kwa upande wake, Balozi wa Ulaya mjini Baghdad amesema Iran ina nafasi muhimu nchini Iraq kwa kuwa ni moja ya nchi muhimu zaidi zinazopakana na taifa hilo la Kiarabu.

Thomas Seiler, Balozi wa EU nchini Iraq amebainisha kuwa, hakuna shaka kuwa kuendelea mazungumzo baina ya maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja Ulaya katika viwango tofauti, kutazaa matunda.

Kadhalika wanadiplomasia hao wawili wa ngazi za juu wa Iran na Ulaya wamebadilishana mawazo kuhusiana na matukio ya hivi sasa kieneo na kimataifa.

 

Tags