Jan 15, 2024 04:31 UTC
  • Matokeo ya Kimbunga cha Al-Aqsa ni dhihirisho la kusimama kidete Muqawama na kutengwa Israel

Baada ya kupita siku 100 tangu Operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa ilipoanza, athari za kusimama kidete harakati za mapambano ya ukombozi au muqawama na kuzidi kutengwa utawala wa Kizayuni wa Israel zinazidi kudhihirika katika maoni ya umma duniani.

Jana tarehe 14 Januari 2024 zilipita siku mia moja tangu makundi ya Muqawama au wapigania ukombozi wa Palestina, yalipotekeleza operesheni dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Tarehe 7 Oktoba 2023, wapiganaji wa Palestina walianza operesheni ya "Kimbunga cha Al Aqsa" ili kukabiliana na jinai na ukatili wa Israel. Operesheni hiyo ilikuwa ya kipekee kwa ukubwa wake wa kijiografia na uwepo mpana wa makundi ya wapiganaji wa Kipalestina. Makundi hayo ya Muqawama yaliushangaza utawala haramu wa Israel kwa hatua yao na utumiaji wa zana mpya za kijeshi. Mafanikio mtawalia ya wapiganaji wa Kipalestina yamewaweka viongozi wa utawala wa Kizayuni katika hali ya kiwewe na kuchanganyikiwa.

Katika siku za mwanzo za Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, utawala wa Kizayuni ulijaribu kubadilisha mkondo kwa faida yake kutokana kipigo ulichopata mikononi mwa harakati za Muqawama. Katika fremu hiyo utawala wa Israel uliweza kupata uungaji mkono wa moja kwa moja wa  Marekani na serikali za nchi za Magharibi.

Pamoja na uwepo wa jeshi la Marekani, lakini mbinu za kitaalamu za Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na matawi ya kijeshi yanayohusiana na harakati hiyo, hasa Brigedi za Izzudin al Qasam, zilifanya hali kuwa ngumu zaidi kwa jeshi la Israel.

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limeshindwa kukabiliana na wapigania ukombozi wa Palestina

Hatimaye mamlaka za utawala wa Kizayuni zililazimika kukubali usitishaji vita katika wiki ya kwanza ya Disemba 2023, jambo ambalo liliashiria nafasi ya juu ya makundi ya ukombozi yya Palestina na kutokuwa na nguvu Wazayuni. Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, ambaye aliahidi ushindi wa haraka na rahisi na hata kuangamizwa Hamas katika siku za kwanza za vita vya Gaza, amekiri kutokuwa na uwezo wa kumaliza vita. Aidha hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel kukiuka mapatano ya usitishaji vita ni kielelezo cha wazi cha sera ya kawaida ya Wazayuni katika kudharau mazungumzo na kukiuka makubaliano.

Aidha katika kipindi hiki cha vita dhidi ya Gaza kumeshuhudiwa kupanuka pengo na hitilafu kati ya viongozi wa utawala wa Kizayuni, na kushadidi maandamano ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel). Halikadhalika katika kipidi hiki cha vita, Mahakama ya Juu ya Israel imetoa hukumu dhidi ya mpango wa Wazayuni wenye misimamo mikali wa kutaka kuongeza nguvu za waziri mkuu wa serikali na pia  "Knesset" (Bunge la utawala wa Kizayuni). Aidha sambamba na kuendelea kwa sera za vita za Netanyahu, matatizo ya kiuchumi yameshadidi huko Israel.

Matokeo ya Operesheni ya Kimbunga cha  Al-Aqsa” hayakomei kwenye masuala ya ndani ya Israel bali pia tunashuhudia taathira zake zisiyo na kifani katika matukio ya kieneo na kimataifa.

Vikosi vya Muqawama vya Yemen katika mlango wa Bahari ya Bab al-Mandeb katika Bahari Nyekundu, katika hatua ya kuwaunga mkono wanamuqawama wa Palestina, vimezuia harakati za meli kuelekea katika bandari zinazokaliwa  kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hatua hiyo ya majeshi ya Yemen imedhihirisha utayarifu wa makundi ya Muqawama katika eneo la Magharibi mwa Asia kukabiliana na muungano wa mara kwa mara wa Wamagharibi na Wazayuni. Katika siku za hivi karibuni, maafisa wa jeshi la Yemen walijibu mashambulizi ya Marekani na waitifaki wa Magharibi wa utawala wa Kizayuni katika Bahari Nyekundu na daima wamesisitiza kwamba wako tayari kusimama kidete na kuwajibu Wazayuni.

Sehemu nyingine muhimu ya matukio ya baada ya Operesheni ya Kimbunga cha  Al-Aqsa imekuwa ni kufedheheka viongozi wa utawala wa Kizayuni na washirika wao katika Ikulu ya Marekani. Idadi kubwa ya watu wamekuwa wakijitokeza mitaani duniani kote  ili kutangaza  uungaji mkono wao kwa watu wa Palestina.

Maandamano ya kuunga mkono Palestina jijini London

Mikusanyiko mikubwa ya waungaji mkono Palestina imeshuhudiwa katika miji ya Ulaya na Amerika Kaskazini. Bila ya shaka kukiri baadhi ya viongozi wa nchi za Magharibi kuhusu jinai zinazofanywa na Wazayuni huko Gaza pia ni matokeo ya mapambano ya makundi ya Wapalestina.

Viongozi wa Ikulu ya White House na wanasiasa wengi wa Marekani siku zote wanatumia rasilimali za kifedha za makundi yanayounga mkono utawala wa Kizayuni kama vile "AIPAC" katika hali ambayo hivi sasa wamekiri kuwepo tofauti kati ya Washington na Tel Aviv kutokana na kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni wa Gaza.

Jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza zimekuwa na taathira kubwa katika fikra za wananchi na nchi huru za dunia kiasi kwamba wengi sasa wameamua "imetosha" na hivyo hawakai kimya tena mbele ya jinai za Israel.

Kuwasilishwa kwa mashtaka ya serikali ya Afrika Kusini dhidi ya viongozi wa utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ni sura mpya katika mielekeo na sera za serikali huru na zisizofungamana na upande wowote ambazo haziko tayari kunyamaza kimya ili kuifurahisha Marekani na madola ya Ulaya.

Uwasilishaji wa mashtaka ya serikali ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni katika mahakama hiyo umekuwa moja ya matokeo muhimu zaidi ya msimamo madhubuti wa mrengo wa wapigania ukombozi wa Palestina katika uga wa kimataifa.

Tags