Mar 27, 2024 06:27 UTC
  • Safari ya pili ya Haniyeh mjini Tehran baada ya operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa

Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, aliwasili Jumanne ya jana mjini Tehran ikiwa ni safari yake ya pili baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ilitekelezwa na wanamuqawama wa Hamas mnamo Oktoba 7, 2023 dhidi ya utawala unaoikalia kimabavu Quds Tukufu. Katika operesheni hiyo, utawala wa Kizayuni ulipata kipigo kikubwa zaidi cha kijeshi na kiintelijensia katika historia yake, kipigo ambacho Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alikitaja kuwa 'kushindwa kusikoweza kurekebishwa.'

Tarehe 5 Novemba takriban mwezi mmoja baada ya operesheni hiyo, Ismail Haniyeh, alifanya safari mjini Tehran, ambapo alikutana na kuzungumza na viongozi wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akiwemo Ayatullah Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Katika mazungumzo hayo Ayatullah Khamenei alisisitiza kwamba siasa za kuunga mkono muqawama wa Palestina ni siasa za kudumu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Moja ya umuhimu wa safari ya mara hii ni kwamba imefanyika siku moja baada ya kupitishwa azimio la Baraza la Usalama kuhusu vita vya Gaza. Hatimaye Jumatatu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliweza kupasisha azimio la kusimamisha vita haraka huko Gaza huku Marekani ikijizuia kulipigia kura ya veto.

Azimio hilo, ambalo lilipitishwa kwa kura za ndio za wajumbe 14 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linataka kusitishwa mara moja mapigano huko Gaza wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, kuandaliwa uwanja wa kufikishwa misaada ya kibinadamu  Gaza na kuachiliwa huru mara moja mateka. Kwa upande mmoja, azimio hilo, halikutaja jina la Hamas, jambo ambalo linaonekana kuwa ni mafanikio ya kisiasa kwa harakati hiyo ya Wapalestina, na kwa upande mwingine, kipengee cha usitishaji vita wa kudumu huko Gaza kiliondolewa kutokana na mashinikizo ya Marekani. Kwa mujibu wa wachunguzi wa masuala ya kisiasa, safari ya Haniyeh mjini Tehran ni muhimu kutokana na kuwa imefanyika siku moja tu baada ya kupitishwa azimio la Baraza la Usalama kuhusu usitishaji vita mara moja.

Haniyeh akizungumza na waandishi habari mjini Tehran

Ismail Haniyeh , Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Hamas amesema katika kikao chake na Hossein Amirabdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kuhusiana kupasishwa hivi karibuni azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba hatua hiyo inaonyesha kutengwa kusiko kwa kawaida utawala wa Kizayuni na kwamba Marekani haina irada na nguvu tena ya kuitwisha Jamii ya Kimataifa matakwa yake, suala ambalo linashiria misimamo thabiti na isiyoyumba ya wananchi na wanamquwama wa Kipalestina katika kukabiliana na utawala haramu na katili wa Israel. Suala jingine muhimu ni kuwa safari hii imefanyika katika kukaribia kufanyika Siku ya Kimataifa ya Quds. Siku ya Kimataifa ya Quds  ni ubunifu uliobuniwa na Imam Khomeini (RA), mwaasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, kwa lengo la kuunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina. Alitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds. Kila mwaka katika siku hii, Waislamu katika nchi nyingi za dunia hufanya maandamano ya kuunga mkono Palestina na kulaani jinai za utawala unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu.

Aidha uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wanamuqawama wa Palestina iwe ni wa Jihad Islami au Harakati ya Hamas umekuwa ukiimarika na serikali ya Iran imekuwa ikiwaunga mkono wananchi wote wa Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake wa Magharibi na tawala za kibaraka za Waarabu. Kuhusiana na suala hilo, Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, mauaji ya kizazi dhidi ya watu wa Gaza yamemuhuzunisha kila mwanadamu aliye na hisia za kiutu na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasita wala kuingiwa na shaka yoyote kuhusiana na usahihi wa msimamo wake imara wa kuunga mkono kadhia ya Palestina na watu wanaodhulumiwa wa nchi hiyo."

Tags