Mar 30, 2024 02:28 UTC
  • Meja Jenerali Bagheri: Jibu la Israel kwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ni mauaji ya watu wasio na hatia

Mkuu wa Majeshi ya Iran amesema kuwa, jibu la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ni kuwaua tu watu wasio na hatia, wakiwemo wanawake na watoto, kuharibu hospitali na kusababisha njaa.

Meja Jenerali Mohammad Bagheri, Mkuu wa Majeshi ya Iran aliyasema hayo jana Ijumaa katika mazungumzo yake na Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), mjini Tehran.

Jenerali Bagheri amesisitiza kwamba operesheni ya kipekee ya "Kimbunga cha Al-Aqsa" ya tarehe 7 Oktoba ilikuwa operesheni kubwa iliyotoa kipigo kikubwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, na kusema kuwa operesheni hiyo ya fahari imebatilisha ngano ya kutoshindwa Israel mtendajinai na kuifanya Palestina kuwa suala la kwanza la Ulimwengu wa Kiislamu na dunia nzima kwa ujumla. 

Mkuu wa Majeshi ya Iran amesema, lau Wamarekani wasingeusaidia utawala wa Kizayuni, Israel ingesambaratika na kushindwa, na jibu la utawala huo kwa kipigo cha wanamapambano wa Palestina ni mauaji ya watu wasio na hatia, wanawake, watoto, kuharibu hospitali na kuwatesa raia kwa njaa.  

Israel imeua maelfu ya watoto wa Palestina

Ameashiria yamapambano yasiyo na kifani wa wananchi wa Palestina dhidi ya mashinikizo ya aina mbalimbali na kuongeza kuwa, watu wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina wameweza kuonesha nguvu ya Uislamu kwa watu wote wa dunia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema masuala mbalimbali yaliwafanya walimwengu wapuuze matakwa ya watu wa Palestina, lakini operesheni ya tarehe 7 Oktoba ilifikisha tena neno la wananchi wa Palestina kwenye masikio ya walimwengu.

Ismail Haniyeh ameeleza kuwa msaada na ufuatiliaji wa vikosi vya jeshi na wananchi wa Iran kuhusiana na masuala ya Palestina unawapa wana jihadi ari kubwa zaidi katika kufanikisha malengo ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa. Vilevile  ameshukuru mazingatio ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, maafisa wa serikali na makamanda wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuendelea kutetea kadhia ya taifa la Palestina.

Tags