Jan 16, 2024 14:27 UTC
  • Kuongezeka uwepo kijeshi wa Marekani huko Iraq na Syria

Marekani ilituma wanajeshi huko Iraq mwaka 2003 wakati ilipoivamia na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo mwaka 2003; na kuhusu Syria pia Marekani ilituma wanajeshi wake nchini humo mwaka 2014 kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi la Kitakfiri la Daesh (ISIS) katika fremu ya Muungano wa Kimataifa wa eti kukabiliana na ugaidi.

Licha ya matakwa ya mara kwa mara ya serikali za Iraq na Syria ya kuondoka majeshi ya Marekani katika ardhi ya nchi hizo, lakini ushahidi unaonyesha kuwa Washington inafanya jitihada za kuzidisha uwepo wake kijeshi katika nchi hizi mbili, hususan baada ya vita vya Gaza na matukio ya kiusalama katika Bahari Nyekundu.  

Washington ilitangaza siku ya Jumatatu kuwa inapanga kutuma wanajeshi wengine 1,500 huko Iraq na Syria ili eti kupambana na kundi la kigaidi la Daesh kufautia mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani huko Syria na Iraq. Inatazamiwa kuwa wanajeshi hao kwanza wataelelekea katika kambi ya polisi ya Fort Bliss katika jimbo la Texas kwa ajili ya kupatiwa mafunzo kabla ya kutumwa katika eneo la Magharibi mwa Asia. Uamuzi wa Marekani wa kutuma kikosi kipya cha jeshi huko Iraq na Syria kwa kile inachokitaja kuwa ni kwa ajili ya kupambana na Daesh umechukuliwa ilhali katika kipindi cha utawala wa rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, Washington ilihusika moja kwa moja katika kulianzisha na kulikuza kundi hilo la kigaidi. Marekani inataka kutuma wanajeshi hao wapya katika hali ambayo tangu kuanza vita Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba mwaka jana, kambi za kijeshi za Marekani huko Iraq na Syria zimeshambuliwa kwa mara zisizopungua 130. 

Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama 

Wakati huo huo serikali za Iraq na Syria, kwa mara kadhaa, zimetaka kuondoka wanajeshi vamizi wa Marekani katika nchi hizo. Kuhusu Iraq, hivi karibuni Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mohammed Shia al Sudani, alitangaza msimamo huo na kulitaka jeshi vamizi la Marekani liondoke nchini humo haraka iwezekanavyo.

Baada ya kuuliwa kigaidi Luteni Jenerali Shahidi Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na Abu Mahdi al Muhandes, Naibu Mkuu wa Harakati ya al Hashdu Shaabi ya Iraq na wanajihadi wenzao katika uwanja wa ndege za Baghdad Januari 3 mwaka 2020, mauaji yaliyotekelezwa na Marekani, Bunge la Iraq tarehe 5 Januari lilipiga kura likitaka kuondoka nchi hiyo vikosi vamizi vya muungano dhidi ya dhidi ya Daesh  wakiwemo wanajeshi wa Marekani katika ardhi ya Iraq. Pamoja na hayo, Marekani imekwenda kinyume ikisisitiza kwamba jeshi lakke litaendelea kuwepo huko Iraq. Hatimaye, kwa kuzingatia mashinikizo ya kisiasa ndani ya Iraq, Rais Joe Biden wa Marekani na Mustafa al Kadhimi Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iraq waliahidi katikati ya majira ya joto mwaka 2021 kwamba kikosi kinachoongozwa na  Marekani huko Iraq kitamaliza majukumu yake kabla ya kumalizika mwaka 2021. 

Bunge la Iraq 

Katika mwaka wa mwisho wa uongozi wa  Donald Trump mnamo 2020, Marekani ilipunguza idadi ya wanajeshi wake nchini Iraq hadi 2,500. Muda wa kuweko vikosi vamizi vya Marekani huko Iraq  kidhahiri ulimalizika Disemba 31 mwaka 2021. Pamoja na hayo, Marekani imeendelea kuwepo kijeshi nchini Iraq kwa anwani nyingine huku ikidhibiti kambi kadhaa za kijeshi kama ile ya Ain al-Asad katika mkoa wa al Anbar na kambi ya Harir katika mkoa wa Erbil. Washington imeendelea kuwepo kijeshi huko Iraq kwa kisingizio cha kutoa ushauri na mafunzo licha ya Bunge la Iraq kupasisha muswada wa kuondoka vikosi vamizi vya Marekani nchini humo. Jambo hilo limekabiliwa na upinzani mkali wa Wairaqi na katika wiki za karibuni kumeshuhudiwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (droni) na makombora dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani huko Iraq na Syria.  

Daesh huko Syria 

Kuhusu Syria pia serikali ya Obama ilianzisha oparesheni za anga na nchi kavu nchini humo mwaka 2014 kwa kisingizio cha mapambno dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) na kuamua kutuma vikosi vamizi vya Marekani nchini humo; katika hali ambayo Marekani yenyewe ndiyo iliyoasisi na inalifadhili kundi hilo la kigaidi. Vilevile Donald Trump, rais wa wakati huo wa Marekani aliendeleza uwepo kinyume cha sheria wa vikosi vamizi vya nchi hiyo huko Syria kwa kisingizio cha kupambana na Daesh na kuanza kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya Syria na kupora mafuta ya nchi hiyo. Vikosi vamizi vya Marekani vipo katika maeneo ya mashariki mwa Syria ambayo yana visima na taasisi za gesi na mafuta na vinaendelea kuiba mafuta ya Syria na kuyavusha kupitia ardhi ya Uturuki.

Hivi sasa pia serikakli ya Biden imedumisha uwepo wa wanajeshi wa nchi hiyo kwa kupuuza kanuni na sheria za kimataifa kama ile inayohusu haki ya kujitawala na pia mamlaka ya umoja wa ardhi nzima ya Syria na bila idhini ya Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Marekani inafanya hivi katika kalibu ya uungaji mkono wake kwa makundi ya kigaidi. Ni wazi kuwa Biden pia anaendeleza sera za mabavu sawa na za Trump mkabala wa mhimili wa Muqawama na Syria.  

Tags